Mpishi Maliha Mohammed azirai akijaribu kuvunja Rekodi ya Dunia ya kupika muda mrefu zaidi

Maliha alikuwa tayari amepika kwa saa 111 na dakika 23 kabla ya kuzirai.

Muhtasari

•Maliha Mohammed alizirai Jumatatu asubuhi alipokuwa kwenye jaribio lake la kuvunja rekodi ya dunia ya muda mrefu zaidi wa upishi.

•Baada ya kuhudumiwa, Mpishi Maliha aliendelea  kupika na akaibishja kwamba amedhamiria kupika kwa saa 200.

azirai akijaribu kuvunja rekodi ya dunia.
Mpishi Maliha Mohammed azirai akijaribu kuvunja rekodi ya dunia.
Image: INSTAGRAM// CHEF MALIHA MOHAMMED

Mpishi wa Kenya mzaliwa wa Pwani, Maliha Mohammed alizirai siku ya Jumatatu asubuhi alipokuwa kwenye jaribio lake la kuvunja rekodi ya dunia ya muda mrefu zaidi wa upishi uliofanywa na mtu binafsi.

Maliha alikuwa tayari amevuka mwendo wa saa 100 kabla ya kuripotiwa kuzirai na kuzimia siku ya Jumatatu asubuhi. Kwa bahati nzuri, madaktari walijibu kwa haraka wakampatia huduma ya kwanza, akaamka tena baada ya muda mfupi na kuendelea na upishi.

Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha wahudumu wa afya wakimhudumia mpishi huyo maarufu ambaye alikuwa amelala kifudifudi.

 

“Mimi ni mshindi na mwanariadha wa mbio za marathoni. Hakuna kinachotuangusha. Hadi mwisho,” Mpishi Maliha Mohammed alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram baada ya kufanikiwa kuamka tena.

Ujumbe wake wa Jumatatu asubuhi ulionyesha kuwa bado amedhamiria kupika kwa saa 200 kama anavyolenga. Mashabiki na wanamitandao wametoa wito kwa Wakenya zaidi kujitokeza katika eneo lake la kupikia ili kumpa sapoti anapojaribu kuvunja rekodi ya dunia.

Kulingana na taarifa yake ya mwisho, Maliha alikuwa tayari amepika kwa saa 111 na dakika 23 kabla ya kuzirai. Hiyo ina maana tayari alikuwa amepita nusu ya muda alioukusudia.

Mpishi Maliha Mohammed anajaribu kuvunja rekodi ya kupika muda mrefu zaidi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Allan Fisher wa Ireland. 

Mapema mwezi huu, Rekodi ya Dunia ya Guiness ilisema kwamba Fisher alipika kwa muda wa saa 119 na dakika 57 katika mgahawa wake nchini Japan, na kuvunja rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na mpishi Hilda ‘Baci’ Bassey wa Nigeria.

Bassey aliweka rekodi hiyo hapo awali Mei mwaka huu baada ya kupika kwa saa 93, dakika 11, hatua iliyomzolea umaarufu mkubwa duniani.