Otile Brown avunja kimya kuhusu tukio la mashabiki kumfokea akiwa jukwaani Raha Fest

"Watu waliokuwa mbele walikuwa wanataka nisogee karibu nao, lakini waliokuwa wameletwa pale ili kunidhalilisha ni wachache, na lile tukio lilikuwa limepangwa kabisa,” Browm alizama Zaidi katika maelezo.

Muhtasari

• Pia msanii huyo alifafanua kuhusu tukio lake kuonekana akiondoka jukwaani na kurudi baada ya sekunde kadhaa huku mashabiki wakizidi kufoka.

Otile Brown
Otile Brown
Image: instagram

Msanii wa kizazi kipya kwa mara ya kwanza amevunja kimya kuhusu klipu inayoenezwa mitandaoni ikimuonyesha akitupiwa maneno na mashabiki akiwa jukwaani wakati wa tamasha la Raha Fest wikendi iliyopita.

Akizungumza na mashabiki wake kwenye kipindi cha mubashara kupitia TikTok, Otile Brown alisema kwamba watu waliomfokea si mashabiki bali ni watu waliolipwa na baadhi ya mahasidi wake kimuziki ili kumdhaliisha.

Pia msanii huyo alifafanua kuhusu tukio lake kuonekana akiondoka jukwaani na kurudi baada ya sekunde kadhaa huku mashabiki wakizidi kufoka.

“Shoo ilikuwa vizuri tu, ni hapo mwanzo tu na ambapo waliichukua na kuikata ikawa vile, kwa sababu nilikuwa nimeambiwa nina dakika 7 za kutumbuiza. Walikuwa na intro yangu na wakati wanaicheza sikuisikia hivyo ikanichochea kurudi nyuma baada ya kugundua sina in-ears kwa sababu sikuwa najisikia,” Otile alifafanua.

“Kwa hiyo kilichotokea ilinibidi niende kuchukua in-ears zangu na watu walikuwa tayari wanafoka. Watu waliokuwa mbele walikuwa wanataka nisogee karibu nao, lakini waliokuwa wameletwa pale ili kunidhalilisha ni wachache, na lile tukio lilikuwa limepangwa kabisa,” Browm alizama Zaidi katika maelezo.

Otile alitumia fursa hiyo kutoa neno moja kwa wale anaodai walipanga njama ya kumdhalilisha kwa kuweka watu sehemu Fulani ili kumpigia kelele akitumbuiza.

Kwa maneno yake, alisema;

“Hao jamaa katika ng’ambo hiyo nyingine, mimi hamniwezi mzee. Sawa, mimi nataka mjue tu, hamniwezi na leo nasema. Na mnajua hiyo ndio maana mnaanza kuungana makundi makundi, kama unajiamini mbona usije twende sawa?”