Eric Omondi amethibitisha kuwania wadhifa wa kisiasa katika uchaguzi wa 2027

“Boti zinakuja, tutapeleka kwa maeneo hatari kama Ruiru, Mathare, baadhi ya sehemu za Kahawa, Thika, Athi River na tatu ziko hapo CBD na pia tuko na mikokoteni 3 tumekodisha kusaidia kuvusha watu kwa maji,” alisema.

Muhtasari

• Akijibu kuhusu baadhi ya watu kumtaka kuacha kamera nyuma wakati anatoa msaada, Omondi alisema kuwa wanaosema hivyo ni wanablogu wa serikali ambao wameewekwa kumpiga vita.

Mwanaharakati Eric Omondi
Mwanaharakati Eric Omondi
Image: Screengrab// YouTube (KOM)

Mchekeshaji aliyegeuka na kuwa mwanaharakati Eric Omondi amethibitisha kujitosa kwenye siasa na kuwania wadhifa wa kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2027.

Akizungumza na Kenya Online Media, Omondi alisema kwamba atajitosa mazima kwenye siasa, na atafanya juu chini kuwaasa vijana wenzake kujitosa kwenye siasa na kuwania nyadhifa mbalimbali.

“Tutawania kwa idadi kubwa na kama hauko debeni tutakuweka kwa nguvu. Tunaenda kuanza kuzungumza kwa vijana, kuwaelimisha, kuwaunganisha pamoja na kuwaandaa kusafisha bunge la Kenya mwaka 2027,” Omondi alisema.

“Wabunge wachache sana watasalia katika bunge, akina Babu Owino, wengine wote tutasafisha. Tutaimba nyimbo, tutaweka mabango, tutasimama, tutaongelesha vijana wasimame kwa sababu kule ndani kumeoza. Kwa hiyo hiyo sio hoja kwa sasa,” Omondi aliongeza.

Akijibu kuhusu baadhi ya watu kumtaka kuacha kamera nyuma wakati anatoa msaada, Omondi alisema kuwa wanaosema hivyo ni wanablogu wa serikali ambao wameewekwa kumpiga vita.

“Sasa hivi ukienda Twitter nilikuwa naona jana tunatrend, wanablogu wa serikali matusi tupu. Wanasema eti Eric Omondi analeta boti kwa maji ambayo kina chake si kirefu. Hao ni wanablogu wa serikali, wanasema ni kiki, wengine wanasema ni kitu tunapanga. Inasikitisha sana,” alisema.

Omondi alisema kwamba suala lake kuzindua mashua za kuwaokoa watu katika sehemu mbalimbali zilizokumbwa na mafuriko litaendelea akiahidi ujio wa mashua Zaidi.

“Boti zinakuja, tutapeleka kwa maeneo hatari kama Ruiru, Mathare, baadhi ya sehemu za Kahawa, Thika, Athi River na tatu ziko hapo CBD na pia tuko na mikokoteni 3 tumekodisha kusaidia kuvusha watu kwa maji,” alisema.