Jaguar amtaka Eric Omondi kufanya kazi na serikali kusaidia wananchi

Jaguar alibainisha kuwa kazi anayofanya Eric Omondi ni ya kupongezwa lakini inaweza kuwa bora zaidi ikiwa ataungana na serikali badala ya kutupia utawala lawama.

Muhtasari

•"Maafa ni makubwa kuliko Eric Omondi," Jaguar alisema

•Ninashukuru kile Eric Omondi anajaribu kufanya, lakini haitaleta matokeo yoyote

Eric Omondi and Jaguar
Image: Hisani

Mwanamuziki mkongwe aliyegeuka kuwa mwanasiasa Charles Njagua Kanyi almaarufu Jaguar anamtaka aliyekuwa mcheshi Eric Omondi kufikiria kufanya kazi na serikali.

Jaguar, ambaye  alikuwa Mbunge wa Starehe kwa miaka 5, alibainisha kuwa kazi anayofanya Eric Omondi ni ya kupongezwa lakini inaweza kuwa bora zaidi ikiwa ataungana na serikali badala ya kutupia serikali lawama.

"Maafa ni makubwa kuliko Eric Omondi," Jaguar alisema.

Aliendelea kubainisha kuwa chochote alichokuwa anafanya mchekeshaji huyo ni kikubwa lakini ana shaka kuwa mtu mmoja anaweza kuleta mabadiliko makubwa.

Katika video inayovuma hivi sasa kwenye Instagram mwanamuziki huyo wa zamani alisisitiza kwamba ikiwa Eric angeungana na serikali basi mabadiliko anayotarajia kuleta yanaweza kupatikana kwa urahisi na bora zaidi.

 

“Nashukuru kwa lolote analofanya lakini sidhani litaleta mabadiliko, binafsi ukiniuliza ni kubwa kuliko yeye naona ni vyema akashirikiana na serikali na kufanya nao kazi ili kuleta mabadiliko," Jaguar alisema waziwazi wakati wa mahojiano aliyokuwa nayo na WanaYouTube.

Jaguar aliendelea kutaja baadhi ya mambo ambayo Eric alifanya hasa wakati huu ambapo taifa limekumbwa na mvua kubwa na mafuriko akiangazia kuwa baba wa watoto 2 hangeweza kuokoa kila mtu hata akitaka.

“Mfano ukiangalia Athi River alikoenda kusaidia watu Kenya nzima inaathirika, ni vizuri ata kama anapiga serikali ashikane na serikali kama anataka kusaidia.

Ninashukuru anachojaribu kufanya, lakini haitaleta mabadiliko yoyote. Haitaleta athari kubwa kwa sababu ni kubwa kuliko chochote anachofikiria,"  Jaquar ilisema.