Barabara 3 za Nairobi na Kiambu zafungwa kutokana na mafuriko - KURA

Pia imeripotiwa kuwa Barabara ya Lang'ata katika eneo la T-Mall haipitiki.

Muhtasari

•KURA ilitangaza kuwa barabara za Enterprise, Eastern Bypass na Thika Bypass ziliathiriwa pakubwa na mvua, jambo ambalo limepelekea hatua ya kufungwa kwa sehemu.

•Mamlaka hiyo pia ilituma onyo kali kwa watumizi wa barabara ikiwataka wasijaribu kuvuka sehemu zilizofurika.

kwenye barabara ya Thika
Mafuriko kwenye barabara ya Thika
Image: HISANI

Mamlaka ya Barabara za Mijini (KURA) imetangaza kufungwa kwa sehemu ya barabara tatu katika kaunti za Nairobi na Kiambu kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Jumanne usiku.

Katika taarifa Jumatano asubuhi, mamlaka hiyo ilitangaza kuwa barabara za Enterprise Road, Eastern Bypass na Thika Bypass ziliathiriwa pakubwa na mvua, jambo ambalo limepelekea hatua ya kufungwa kwa sehemu.

Walisema kuwa polisi wa trafiki na timu yao ya kiufundi tayari walikuwa uwanjani kuwaelekeza watumiaji wa barabara na kuimarisha usalama wao.

“Kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jana (Jumanne) usiku kote nchini, barabara zifuatazo katika Kaunti za Nairobi na Kiambu zimeathirika pakubwa na kusababisha kufungwa kwa kiasi; Barabara ya Enterprise, Eastern bypass na Thika bypass,” KURA ilisema kwenye taarifa.

Mamlaka hiyo pia ilituma onyo kali kwa watumizi wa barabara ikiwataka wasijaribu kuvuka sehemu zilizofurika.

 "Polisi wa trafiki na timu yetu ya kiufundi wako uwanjani kuelekeza trafiki na kuimarisha usalama wa Madereva. Tutaendelea kuwajuza kadri hali inavyoendelea. Tafadhali endesha kwa usalama na USIjaribu kuvuka sehemu zilizofurika,” KURA ilisema.

Haya yanajiri wakati barabara mbalimbali nchini Kenya zikiripotiwa kujaa maji kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Pia imeripotiwa kuwa Barabara ya Lang'ata katika eneo la T-Mall haipitiki. Sehemu hiyo imefungwa kutokana na mafuriko makubwa. Wenye magari wanashauriwa kutafuta njia mbadala.