Idara ya utabiri wa hali ya anga yatangaza maeneo yatakayoshudia mvua leo, Jumapili

Met ilitangaza utabiri wa hali ya hewa wa Jumapili ikifichua kuwa sehemu mbalimbali za nchi zitashuhudia viwango tofauti vya mvua.

Muhtasari

•Idara ilisema kuwa mvua ndogo ya milimita 5 hadi mvua ya wastani ya 5mm-20mm itanyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi.

•Pia walitahadharisha kuhusu mvua kubwa ya kutoka milimita 20 hadi zaidi ya milimita 50 katika maeneo kadhaa ya nchi.

Image: BBC

Jumamosi jioni, Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ya Kenya (Met) ilitangaza utabiri wa hali ya hewa wa Jumapili ikifichua kuwa sehemu mbalimbali za nchi zitashuhudia viwango tofauti vya mvua.

Idara ilisema kuwa mvua ndogo ya milimita 5 hadi mvua ya wastani ya 5mm-20mm itanyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Pia walitahadharisha kuhusu mvua kubwa ya kutoka milimita 20 hadi zaidi ya milimita 50 katika maeneo kadhaa ya nchi ikiwa ni pamoja na maeneo ya Kati, Nairobi, Bonde la Ufa na Pwani.

"Utabiri wa mvua wa Jumapili: ☔ Mvua nyepesi (<5mm) hadi Wastani (5-20mm) inatarajiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Mvua Zilizotengwa Nzito (milimita 20-50) hadi Nzito Sana (>50mm) huenda zikanyesha katika baadhi ya maeneo ya Kati, Nairobi, Kusini-mashariki, Bonde la Ufa na maeneo ya Pwani. Kaa tayari!,” Met alisema Jumamosi jioni.

Idara hiyo ya utabiri wa hali ya anga mnamo Jumatano ilionya kuhusu mvua kubwa ambayo ingenyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia Alhamisi, Mei 2, hadi Jumapili ya Mei 5.

Kufuatia hali hiyo, idara hiyo iliwataka wakenya kuwa waangalifu zaidi huku mvua hiyo kubwa ikishuhudiwa katika maeneo mbalimbali.

"Tazamia kuongezeka kwa kiwango cha mvua katika maeneo mengi ya nchi kuanzia Alhamisi hadi wikendi. Kaa salama na mkavu, kila mtu!” Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ya Kenya ilionya.

Idara hiyo ilitaja maeneo mbalimbali ya nchi ya Kenya ambayo yalitarajiwa kushuhudia mvua kubwa katika siku zijazo.

Maeneo hayo ni pamoja na Nyanda za Juu Mashariki/Magharibi mwa Bonde la Ufa, Eneo la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Maeneo ya Nyanda za Juu Kusini-mashariki, na maeneo ya Kaskazini-magharibi na Kaskazini-mashariki.

Siku ya Jumatano, Papa Francis alituma ujumbe wa kuwafariji Wakenya wakati nchi  ikikabiliwa na mafuriko makubwa.

Katika ujumbe wake wa siku ya Jumatano, 1 Mei 2024, Papa alitoa wito wa kuiombea nchi ya Kenya wakati wananchi wanakabiliana na makali ya mafuriko.

Alisema kwamba yeye binafsi anawaombea Wakenya ambao wanakabiliwa na athari za mafuriko ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya takriban watu 200.

"Niko karibu kiroho na watu wa Kenya wakati huu ambapo mafuriko makubwa yamegharimu maisha ya watu wengi na kuharibu maeneo makubwa. Tuwaombee kwa pamoja wale wote wanaopatwa na maafa haya ya janga," Papa alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X.

Haya yanajiri kufuatia mafuriko yanayoendelea nchini ambayo yamesababisha uharibifu wa maisha na mali.