Serikali ya Nairobi yafichua hali ya wapangaji wa nyumba ya Uthiru iliyoporomoka

"Jengo lilikuwa linazama polepole, na wakazi wote waliweza kuruka nje na kufanikiwa kutoka nje ya jengo hilo," Simiyu alisema.

Muhtasari

•Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Majanga wa Nairobi Bramwel Simiyu alisema hakuna maafa ambayo yameripotiwa kutokana na kisa hicho.

•Simiyu alisema kuna nyumba moja yenye moto wa gesi ambayo iliruhusiwa kuteketea kwa usalama.

Mandhari ya jengo lililoporomoka, Mei 7, 2024.
Mandhari ya jengo lililoporomoka, Mei 7, 2024.
Image: HISANI

Wakaazi wote 34 wa jengo lililoporomoka katika Wadi ya Mountain View kaunti ya Nairobi, eneo la Uthiru, wamepatikana na wako salama, serikali ya Kaunti ya Nairobi imesema.

Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Majanga wa Nairobi Bramwel Simiyu alisema hakuna maafa ambayo yameripotiwa kutokana na kisa hicho.

Aliondoa hofu kuhusuwakaazi wanne ambao walikuwa wametoweka ambao awali walijumuisha msichana wa miaka 10, alisema wasiwasi huo umeondolewa.

"Jengo lilikuwa linazama polepole, na wakazi wote waliweza kuruka nje na kufanikiwa kutoka nje ya jengo hilo," Simiyu alisema.

Hata hivyo, alisema timu ya dharura ya serikali ya kaunti itaendelea kuzunguka eneo hilo huku wakisubiri Usaidizi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya kutoka Kahawa Barracks kupeleka mbwa wao wa kunusa ili kubaini uwezekano wa mtu kunaswa kwenye vifusi.

Simiyu alisema kuna nyumba moja yenye moto wa gesi ambayo iliruhusiwa kuteketea kwa usalama.

"Serikali ya Kaunti ya Jiji la Nairobi inatoa msaada wa haraka wa kibinadamu kwa usiku huo na inapanga kutoa usaidizi zaidi na kuwezesha kuunganishwa tena," alisema.