Ruben Amorim: Kocha wa Sporting Lisbon ajitenga na madai ya kukubali kuifunza Liverpool

Akizunumza na waandishi wa habari, Mreno huyo mwenye umri wa miaka 39 amekanusha vikali tetesi zilizokuwa zinamhusisha na Liverpool.

Muhtasari

• Amorim alisema hajawahi kutana na Liverpool wala kuwa na mazungumzo yoyote nao kama ambavyo ilivyoripotiwa na vyombo vya habari Uingereza siku chache zilizopita.

RUBEN AMORIM
RUBEN AMORIM
Image: HISANI

Kocha wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim anayepigiwa upatu kuwa mrithi wa Mjerumani Jurgen Klopp katika klabu ya Liverpool amejitenga na madai ya kukutana na uongozi wa miamba hao wa Uingereza.

Akizunumza na waandishi wa habari, Mreno huyo mwenye umri wa miaka 39 amekanusha vikali tetesi zilizokuwa zinamhusisha na Liverpool.

Amorim alisema hajawahi kutana na Liverpool wala kuwa na mazungumzo yoyote nao kama ambavyo ilivyoripotiwa na vyombo vya habari Uingereza siku chache zilizopita.

Alisisitiza kwamba bado yeye ni kocha wa Sporting CP na hilo ndilo analojua kwa sasa.

"Sikukutana na Liverpool kwa mahojiano yoyote na hakuna makubaliano, sio kweli. Mimi ni meneja wa Sporting, nataka kushinda hapa na sikukutana na klabu yoyote. Hakuna kilichokubaliwa. Achana na hadithi hii. Hii ni mara ya mwisho nazungumza kuhusu maisha yangu ya baadaye."

Mwanahabari wa Sky Sports, Florian Plettenberg alidai mapema wiki hii kwamba kulikuwa na makubaliano ya mdomo kati ya Liverpool na Amorim huku pande zote mbili zikitarajia kupata makubaliano haraka iwezekanavyo.