Jeremy Doku athibitisha kujihisi kuwa Mghana licha ya kuchagua uraia wa Ubelgiji

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alizaliwa mjini Antwerp, Ubelgiji kwa wazazi wenye asili ya Ghana na aliwakilisha Ubelgiji katika ngazi ya vijana kutoka U-15 hadi U-21.

Muhtasari

• Alipoulizwa kuhusu asili yake ya Ghana, Doku alikiri asili ya wazazi wake na kusema pia anazungumza Lugha ya Twi.

Jeremy Doku
Jeremy Doku
Image: Hisani

Nyota wa Manchester City, Jeremy Doku amethibitisha kuwa anajihisi Mghana licha ya kuchagua kuichezea Ubelgiji katika ngazi ya kimataifa, akisisitiza kuwa hata anazungumza lugha ya Twi, maarufu katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alizaliwa mjini Antwerp, Ubelgiji kwa wazazi wenye asili ya Ghana na aliwakilisha Ubelgiji katika ngazi ya vijana kutoka U-15 hadi U-21.

Doku alikuwa kwenye rada za Chama cha Soka cha Ghana (GFA) wakati fulani lakini akachagua kuiwakilisha Ubelgiji katika ngazi ya juu na akaichezea Red Devils katika mchezo wa UEFA Nations League dhidi ya Denmark Septemba 2020.

Aliendelea kuichezea Ubelgiji kwenye Euro 2020 na tangu wakati huo amecheza mechi 20 kwa taifa hilo la Ulaya huku akichangia mabao mawili.

Alipoulizwa kuhusu asili yake ya Ghana, Doku alikiri asili ya wazazi wake na kusema pia anazungumza Lugha ya Twi.

"Kwa kweli, mimi ni Mghana pia kwa sababu wazazi wangu ni Waghana. Pia ninazungumza Kitwi, ambayo ni lugha nchini Ghana. Nimewahi huko mara moja na itabidi nirudi huko tena kwa sababu ilikuwa muda mrefu uliopita,” Doku alisema kwenye kipindi cha The Premier League Chair show.

Doku alijiunga na Manchester City akitokea Stade Rennes ya Ligue 1 msimu uliopita wa joto na amekuwa na msimu mzuri na kikosi cha Pep Guardiola hadi sasa.

Akipima muda wake na Cityzens, winga huyo alisema anaamini ametulia vizuri lakini akaongeza kuwa kuna nafasi ya kuboresha.