18 waangamia, 172 wakilazwa hospitalini baada ya lori la mafuta kulipuka

Yamkini watu 18 wamethibitishwa kuaga dunia na wengine 172 wakiuguza majeraha hospitalini baada ya lori la mafuta kulipuka katika mji wa Wenling nchini China mkoa wa kaskazini wa Zhejiang.

Lori hilo lilikuwa linasafirisha gesi(LNG) wakati lilishika moto na kulipuka siku ya Jumamosi, Juni 13.

Kulingana na CGTN News Mlipuko huo ulipeleka nyumba na viwanda vilivyokuwa karibu kuanguka na kufunikwa kwa wingu jeusi la moshi na kuharibu magari kadhaa.

Baada ya kushika mto, lori hilo lilipoteza mwelekeo na kuingia katika duka lililokuwa karibu na kusababisha mlipuko. Video iliyosambazwa na shirika hilo la habari inaonyesha moto mkubwa huku watu wakipiga kamsa.

Katika video moja, vifusi vikubwa vinaonekna vikipepea hewani kabla ya kuangukia majengo yaliyokuwa mkabala.

Video nyingine inaonyesha mabaki ya lori hilo na magurudumu kadhaa yaliyogonga majengo ambayo yalikuwa yamegeuka kuwa vifusi. Shughuli za uokoaji zinaendela huku kufikia Jumapili asubuhi maafisa wa usalama walisema kikosi cha matabibu 600 kimetumwa kuwashughulikia walioathiriwa.