Rais wa Venezuela afanya mazungumzo na rais wa Marekani

_108387863_055849929-1
_108387863_055849929-1

Raisi wa Venezuela Nicolás Maduro amesema yupo kwenye mazungumzo na utawala wa raisi Donald Trump kwa miezi kadhaa sasa - licha ya vikwazo vipya vya Marekani kwa taifa hilo.

Mgogoro unaoedelea wa kisiasa na kiuchumi umeianya Venezuela kuwa na marais wawili waliojitangazia uhalali wa kuongoza.

Marekani ni moja ya mataifa 50 ambayo hayamtambui Maduro kama raisi halali wa Venezuela.

Utawala wa Washington ulitangaza vikwazo vipya dhidi ya Venezuela mwanzoni mwa mwezi kama njia ya kumuongezea Maduro shinikizo la kung'atuka.

Hata hivyo jana Jumanne, Maduro amethibitisha kuwa amekuwa kwenye mazungumzo na maafisa waandamizi wa serikali ya Trump kwa miezi kadhaa sasa.

Akizungumza kupitia runinga, Maduro amesema: "Kama nilivyofanya mazungumzo ndani ya Venezuela, pia nimetafuta namna ya kumfanya raisi Trump aisikilize Venezuela."

Raisi Trump pia amethibitisha kuwa utawala wake umekuwa kwenye "mazungumzo na wawakilishi wa Venezuela".

"Sitaki kusema nani, lakini tunazungumza na watu wa ngazi ya juu kabisa," amesema Trump.

Hali ikoje Venezuela

Taifa hilo limekabiliwa na mgogoro wa uongozi kati ya rais Maduro na kiongozi wa bunge la Venezuela , Juan Guaidó.

Bwana Guaidó alijitangaza mwenyewe kuwa kaimu rais mnamo mwezi Januari , akidai kwamba uchaguzi uliomleta maduri uongozini kwa muhula wa pili ulikumbwa na udanganyifu.

Huku Bwana Guaido akiungwa mkono na mataifa 50, ameshindwa kumng'oa madarakani bwana Maduro.

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalioandaliwa Barbados na kuongozwa na Norway yaligonga mwamba baada ya rais Maduro kuupinga upinzani kwa kuunga mkono vikwazo vilivyowekwa na Marekani.

Taifa hilo linakumbwa na mdororo mbaya zaidi wa kiuchumi huku robo ya idadi yake ya watu milioni 30 ikihitaji msaada kulingana na Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya raia milioni 4 wa Venezuela wameondoka katika taifa hilo katika kipindi cha miaka iliopita.