Uteuzi wa mbunge wa zamani wa Othaya Mary wambui kama mwenyekiti maamlaka ya ajira umezua lalama kali sana mtandaoni kutoka kwa wakenya na hasa katika ukumbi wa twitter .wengi wamehoji nia ya serikali kumpa wambui kazi hiyo kwani suala la ajira linazua hisia kutoka kwa vijana wengi nchini ambao wamezua shauku iwapo wambui ana uwezo wa kutoa na kutekeleza sera na mikakati bunifu ya kuwawezesha vijana kupata kazi .waziri wa leba Ukur Yattani alitangaza uteuzi wa wambui katika maamlaka hiyi kupitia arifa maalum ya gazeti rasmi la serikali hapo jana .
Mwanamikakati wa mawasiliano wa kidijitali Dennis Itumbi na shahidi Samuel gateri wameshtakiwa upya kuhusiana na barua feki iliyodai kuwepo njama ya kumwua naibu wa rais William Ruto . wawili hao wamefikishwa kortini leo baada ya upande wa mashtaka kuziunganisha kesi zao . wamekanusha mashtaka ya kuchapisha taarifa ya wongo kinyume cha sheria .
Mkurugenzi wa mashtaka ya umma amewasilisha kesi ya ukiukaji wa agizo la mahakama dhidi ya mjane wa TOB COHEN SARAH WAIRIMU NA wakili wake Philip Murgor . DPP anasema wawili hao wanafaa kuchukuliwa hatua kwa kuzungumzia mauaji ya COHEN wakati wa maazishi yake .
Afisi ya mratibu wa bajeti imekashifiwa leo na maseneta kuhusu kutolewa kwa pesa kwa njia isiofaa kwa ununuzi wa vifaa vya matibabu katika hospitali za umma . aliyejipata pabaya ni kaimu mratibu wa bajeti Stephen Masha .
Bunge la kaunti ya meru leo linajadili mswada wa punguza mizigo .mswada huo hadi kufikia sasa umekataliwa na kaunti 16 na ni uasin Gishu pekee ndio iliyoupitisha .
Rais wa zamani wa afrika kusini Jacob Zuma atakata rufaa katika kesi ya ufisadi dhidi yake baada ya mahakama wiki jana kutupilia mbali ombi lake kwamba kesi hiyo ifutiliwe mbali . Madai ya ufisadi dhidi ya Zuma ni ya miaka ya 90 wakati taifa hilo lilipotoa kandarasi ya ununuzi wa sulaha .Hilo linajiri baada ya marekani wiki jana kuiwekea vikwazo familia ya Gupta na mshirika wao mmoja kwa tuhuma za ufisadi nchini afrika kusini . Familia ya Gupta ilikuwa na uhusiano wa karibu na Zuma na utawala wake.