Ruto aanza mikutano ya mashinani, Ijumaa atakuwa Mombasa

Ruto na Raila
Ruto na Raila

Naibu rais William Ruto ameamua kupeleka mikutano yake mashinani na amegawa mikutano hiyo katika maeneo manane kote nchini katika kile kinachoonekana kama mikakati ya kuimarisha umaarufu wake mashinani tayari kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Tangu kupigwa marufuku kwa mikutano ya umma ili kukabili usambaaji wa virusi vya corona, Ruto amekuwa akikutana na wafuasi wake katika makaazi yake mtaani Karen mjini Nairobi na nyumbani kwake Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu.

Soma habari zaidi;

Katika mikutano ya Karen naibu rais amekuwa mwenyeji wa mamia ya wafuasi wake kutoka kaunti za Nairobi, Murang'a, Kiambu, Nyeri, Kirinyaga na Kajiado miongoni mwa makundi mengine.

Ijumaa hii, Ruto atakuwa Mombasa kwa ziara ya siku mbili ambapo atafanya mikutano kadhaa. Anatarajiwa kukutana na viongozi waliyochaguliwa, viongozi wa kidini, jamii, vijana na wataalam kutoka kaunti zote sita za Pwani; Mombasa, Taita Taveta, Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River.

Soma habari zaidi;

Eneo la Pwani kwa muda mrefu limekuwa likimuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga.

Mbunge wa Nyali Mohamed Ali aliambia kwamba Ruto ataenda kukutana na wananchi wa Pwani na kuwasikiza.

“Utakuwa msafara mkubwa Ruto atakapowasili hapa. Chamsingi ni shughuli tu ya wapwani na hakuna siasa," Mbunge huyo wa Nyali alisema kwa njia ya simu.

"Tunazungumzia mambo yetu. Ni mtu mzuri na atatusikiza. Sisi ni taifa la walala hoi na idadi yetu yaongezeka.”

Mbunge huyo alisema kwamba Mombasa imetelekezwa sana na wananchi wanaumia, "tunataka barabara, shule nzuri, hospitali nzuri lakini wale katika serikali kuu wametusahau,".