Abby mwanawe naibu wa Rais William Ruto, afanya vyema KCPE 2019

Mwanawe Naibu wa Rais William Ruto amepata alama 406 katika matokeo ya mtihani wa KCPE.

Abby Cherop Ruto alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliotia fora sana katika shule ya msingi ya Greenvale iliyoko kaunti ya Uasin Gishu.

Mamake, Prisca Chemutai Bett, alisema kwamba bintiye amekuwa mwenye bidii sana katika masomo yake.

Aidha alisema kwamba shukran za mafanikio yake yanamwendea naibu wa Rais William Ruto ambaye amekuwa msaidizi.

"Ninajua amepokea taarifa hizo. Lakini bado hajatuma ujumbe wa kumpongeza na ninaamini atatuma atakapopata muda. Amekuwa akitusaidia na ninapongeza juhudi zake,"  Chemutai alisema.

Chemutai alisema ingawa yu ngali anachambua matokeo, lakini anaamini kwamba Abby Ruto ni miongoni mwa wanafunzi tano bora.

Jumla ya wanafunzi 1,083,465 walifanya mtihani wa KCPE 2019. Kati ya hiyo, 543,582 ni wanaume huku 539,874 wakiwa wasichana.

Mnamo 2017, Chemutai alitaka korti imwamuru Naibu wa rais Ruto kumpa malezi bora.

Alimshtumu kwa kumtekeleza yeye pamoja na mwanawe huku wakilalamikia kuishi katika ufukura baada ya kudai kuwa Ruto alikuwa ameacha majukumu yake.

Chemutai alidai kuwa Ruto alikuwa mpenziwe wa kitambo.

"Mwanangu wa umri wa miaka 11, Abby anapata malezi bora kutoka kwangu ikiwemo masomo katika shule ya msingi ya kibinafsi," Ruto alisema kupitia Twitter.

Aidha alisema kuwa suala hilo lilikuwa limechochewa kisiasa.