AFCON 2019: Rais Uhuru Kenyatta aipongeza timu ya Taifa ya Soka Harambee Stars kwa kufuzu kuingia michuano

Rais Uhuru Kenyatta ameipongeza timu ya Taifa ya Soka Harambee Stars kwa kufuzu kuingia kwa michuano ya Mataifa Bingwa Barani Afrika mwaka 2019.

Rais alisema kufuzu kwa timu ya Taifa kwa kinyanganyiro hicho barani kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 15 ni ufanisi wa kusisimua kwa wapenda soka nchini na akatoa hakikisho wa kuiunga mkono kikamilifu timu hiyo.

“Ufanisi wa timu yetu ya Taifa ni ishara ya mabadiliko katika michezo yetu. Tunajivunia kile vijana wetu wanafanya kuimarisha viwango vya mchezo huo nchini,”kasema Rais Kenyatta.

Thibitisho kwamba Timu ya Taifa Harambee Stars imefuzu kwa michuano hiyo ya Mataifa Bingwa Barani Afrika mwaka wa 2019 lilitangazwa siku ya Ijuma baada ya kikao kisicho cha kawaida cha siku nzima cha Kamati Kuu ya Shirikisho la kandanda Barani Afrika (CAF) Jijini Accra, Ghana, kubainisha uamuzi kuhusu timu ya taifa ya Sierra Leone.

Sierra Leone, ambayo ilikuwa katika kundi la F la kufuzu pamoja na Kenya, Ghana na Ethiopia haijashiriki michezo yake mitatu ya mwisho baada ya chama chake cha Soka kupigwa marufuku na Shirikisho la soka duniani FIFA.

Huku ikiwa imesalia  mechi moja ya makundi kukamilika, Shirikisho la CAF liliafikia uamuzi wa kufutilia mbali matokeo yote yaliyohusisha taifa hilo la Afrika Magharibi na hivyo kuliacha kundi hilo na timu tatu pekee.

Sierra Leone ilikuwa imecheza tu mechi mbili katika kampeini yao na kwa sababu haikuwa imekamilisha nusu ya mechi zote za kufuzu, Shirikisho la CAF liliamua kufutilia mbali matokeo yote ya awali yaliyohusisha taifa hilo kulingana na kanuni za kufuzu.

Rais Kenyatta alisema Serikali kupitia Wizara ya Michezo itaendelea kuiunga mkono timu ya Taifa ya Soka inapojiandaa kwa kindumbwe-ndumbwe hicho Barani.

“Tunajua mnaweza kushinda taji hili. Nawahakikishia usaidizi wangu na Serikali itafanikisha na kuwapa rasilimali zinazohitajika kuhakikisha mumejiandaa viivyo kwa kazi iliyo mbele yenu,” Rais Kenyatta alihakikisha.

Mapema Waziri wa Michezo Rashid Echesa, kupitia kitandazi chake cha Twita aliipongeza timu ya taifa kwa kufuzu.

"Kinyang’anyiro hiki kimetuhepa kwa muda wa miaka 15. Nawashukuru vijana wetu kwa kupambana vilivyo dhidi ya timu zote katika kundi lao na kufuzu kuiwakilisha Kenya," Waziri alisema.

Katibu katika Wizara ya Michezo, Balozi Kirimi Kaberia alisema wanamichezo wa Kenya waume kwa wanawake ni raslimali muhimu ya taifa na akaiihimiza timu ya hiyo  ya Soka Harambee Stars kulenga ufanisi katika kinyanganyiro hicho.

Alisema marekebisho mengi yaliyoanzishwa na Serikali na usaidizi kutoka kwa Rais Kenyatta, sekta ya michezo imeshuhudia mabadiliko makubwa yanayowapa viajana wa Kenya matumaini ya kuboresha talanta zao.

Katibu Kaberia alisema maendeleo yanayojiri ya miundomsingi katika vifaa vya michezo ikiwemo ukarabati wa uwanja wa Taifa wa Nyayo ambao ni wa pili kwa ukubwa ni ishara kuhusu kile Serikali imeamua kufanya kuhakikisha vijana wa Kenya wanabobea katika michezo.

Also read more here