Afueni kwa Waiguru! Mahakama ya juu yaidhinisha uchaguzi wake

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amepata afueni baada ya mahakama ya Upeo siku ya Jumanne kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na kinara ya Narc Kenya Martha Karua kupinga uchaguzi wake wa mwaka 2017.

Mwezi Agosti mwaka 2018, Karua alipoteza kesi baada ya mahakama ya rufaa kushikilia uamuzi wa mahakama kuu kutupilia mbali kesi ya kupinga uchaguzi wa Waiguru.

Katika uamuzi wake Jaji wa mahakama ya upeo Isaac Lenaola pia aliagiza kuwa kila upande usimamiye gharama zake za kesi kutoka mahakama kuu, mahakama ya rufaa na katika mahakama ya upeo.

Karua aliwasilisha kesi katika mahakama ya rufaa wiki moja baada ya mahakama kuu mjini Kerugoya kutupilia mbali kesi yake iliyokuwa ikipinga uchaguzi wa Waiguru.  Alikuwa amepinga uamuzi wa mahakama kuu ya Kerugoya iliopuuzilia mbali ombi lake.

Jaji Lucy Gitari alitupilia mbali kesi hiyo kwa misingi kwamba ilikosa mashiko na kumuagiza alipe gharama za kesi hiyo shilingi milioni tano. Kinara huyo wa Narc Kenya aliwania ugavana wa Kirinyaga katika uchaguzi wa mwaka 2017 lakini alilambishwa vumbi na Waiguru aliyezoa kura 153,353 huku Karua akipata kura 116,626 naye aliyekuwa Gavana Joseph Ndathi akipata kura 4,496.