Afueni kwa watoa ushuru, Uhuru apunguzia wakenya ushuru kutokana na athari za corona

Athari za virusi vya corona zimeanza kudhihirika huku serikali ikilazimika kufanyia mabadiliko mfumo wake utozaji ushuru. Ni afueni kwa wakenya watoa ushuru baada ya rais Uhuru Kenyatta kutangaza kupunguzia wakenya ushuru ili kuwakinga wananchi kutokana na athari za virusi vya corona.

Wafanyikazi wote wanaopata mshahara wa shilingi 24,000 kwenda chini hawatatozwa ushuru wowote kwa mishahara yao. Rais Kenyatta vile vile ametangaza kupunguza ushuru wa mapato (PAYE) kwa wafanyikazi wengine wanaopata mishahara ya zaidi ya shilingi 24,000 kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25.

Sekta za kibinafsi pia hazijaachwa nje kwani serikali imewapunguzia mzigo wa ulipaji ushuru kuanzia kwa makampuni makubwa hadi wafanyibiashara wadogo wadogo. Wananchi wote kwa jumla pia wana sababu ya kutabasamu baada ya rais Kenyatta kutangaza kupunguza ushuru wa ubora wa bidhaa (VAT) kutoka aslimia 16 hadi asilimia 12.

Akitangaza mabadiliko hayo, rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba lengo kuu ni kuhakikisha kwamba waajiri wanapewa kinga ili wasilazimike kupunguza wafanyikazi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi. Anasema serikali itaendelea kuweka mikakati kulinda nafasi za kazi nchini pamoja na kuhakikisha kwamba wananchi hawaumii.

Ili kuweza kufanikisha mipango ya serikali rais Kenyatta vile vile ametangaza kupunguza mishahara ya maafisa wa ngazi za juu katika serikali. Mshahara wa rais na naibu wake utapunguzwa kwa asilimia 80, mshahaha wa mawaziri utapunguzwa kwa asilimia 30, huku mshahara wa makatibu wa kudumu na maafisa wengine wakuu wa idara za serikali ukupunguzwa kwa silimia 20.