Aisha Jumwa aonyeshwa kivumbi Ganda, ODM yatamba

Reuben Katana mgombea wa chama cha ODM ndiye mshindi katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda katika kaunti ya Kilifi.

Katana alibwaga wapinzani wake kwa kuzoa jumla ya kura elfu 4,177.

Uchaguzi huo mdogo wa wadi ya Ganda katika kaunti ya Kilifi ulifanya siku ya Alhamisi.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo siku ya Ijumaa, afisa msimamizi wa uchaguzi Juma Musa, alisema Katana alipata kura nyingi kuliko mgombea yeyote yule katika uchaguzi huo.

Abdul Omar ambaye ni muaniaji huru na ambaye alikuwa akipigiwa debe na Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa alikuwa wa pili kwa jumla ya kura 2,331.

Mgombea wa Jubilee Joseph Kiponda akipata kura 599 huku David Mitsanze wa KADU Asili akipata kura 362.

Akitoa hutuba yake dakika chache baada ya kutangazwa mshindi, Katana alipongeza tume ya IEBC kwa kuendesha uchaguzi huru na haki, huku pia akishukuru idara ya polisi kwa kudumisha amani.

Katana aliwasihi wapinzani wake kuungana naye kwa lengo la kuleta maendeleo na kushukuru wakaazi wa eneo kwa kuwa na imani naye.