Aisha Jumwa atiwa mbaroni kuhusiana rabsha Malindi

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Malindi kuhusiana na ghasia zilizotokeo katika eneo la Ganda na kupelekea mtu mmoja kuauwa.

Ngumbao Jola alifariki baada ya kupigwa risasi kifuani kutokana na rabsha zilizofuatia.

Aisha alikamatwa pamoja na watu wengine wanne usiku wa manane na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Malindi.

Polisi walikuwa na wakati mgumu kumtia mbaroni Aisha baada ya mbunge huyo kudinda kufungua lango la kuingia nyumbani kwake na kuwalazimu kulivunja kabla ya kumkamata.

Aisha na wafuasi wake wanadaiwa kuvamia mkutano wa ODM uliokuwa ukifanyika nyumbani kwa mgombea wa kiti cha uakilishi wadi cha Ganda kwa tiketi ya ODM Reuben Katana.

Aisha alidai kuwa ODM ilikuwa inaendelea na kampeni licha ya muda wa kufanya hivyo kukamilika.

Aisha anatarajiwa kufikishwa mahakamani punde tu uchunguzi utakapokamilika.