Ajuza wa miaka 63 ajifungua mtoto Uganda baada ya ndoa ya miaka 47

ajuza
ajuza
Safinah Namukwaya alipoolewa na Badru Walusimbi, mkazi wa kijiji cha Nunda huko Lwabenge, katika kitongoji cha Kalungu mwaka 1996, nia yake kuu ilikuwa ni angalau kujifungua mtoto mmoja. Licha ya kuolewa kwa miaka 24, Namukwaya alikuwa hajabarikiwa na watoto.

Jitihada za kupata mtoto zilianza kuanzia kwa mwanaume wa kwanza aliyemuoa mwaka 1973 na kuishi naye mpaka 1987, alikuwa anasumbuliwa na tatizo la uzazi kwa mayai kushindwa kukua ndani ya mfuko wa uzazi. Mnamo Machi 2019, wakati anatimiza miaka 63, alitembelewa na wataalamu wa afya ya uzazi ' Women's Hospital International and Fertility Centre' huko Bukoto, Kampala na kufanyiwa uchunguzi na Dkt Edward Tamale Ssali, ambaye alimweleza kuwa anaweza kujifungua licha ya umri wake kuwa umesonga.

Miezi kadhaa baadaye, alipata ujauzito na siku ya Alhamisi (Juni 25, 2020), Namukwaya alijifungua mtoto katika hospitali ya mkoa ya Masaka.

Daktari wa Hospitali kuu ya wilaya ya Masaka Dkt. Herbart Kalema Alifahamisha gazeti la udaku la Red Ppepper kwamba mama huyo alipata matatizo wakati wa ujana wake alipopata mimba lakini walimfanyia upasuaji ambao ulifanyika kimakosa na kusababisha kushindwa kuzaa tena.

Hata hivyo Dkt. Kalema ameongeza kwamba mama huyo alifanyiwa upasuaji baada ya kukuta mtoto amezungukwa na maji mengi kabla ya kufikisha miezi tisa za kujifungua, mtoto akiwa na miezi minane.

Kulingana na Dkt. Kalema, hali ya mtoto ni nzuri pamoja na mama yake ila mtoto watamtunza kwa majuma matatau kabla ya kuruhisiwa kwenda nyumbani.

Anasema gharama yote inagharimu shilingi milioni 15 za Uganda lakini Namukwaya alishindwa kupata fedha hizo hivyo alitakiwa kulipa shilingi milioni 4 za Uganda.

"Hospitali iliweza kuongezea kiasi cha fedha kilichosalia ili kumfanya mama huyo apate mtoto," mkurugenzi wa hospitali aliongeza.

Dkt Ssali alisema mwanamke yeyote anayekaribia kufika miaka 70 ana uwezo mkubwa wa kuweza kuzaa bado, kwa kusaidiwa kupata mbegu za mume wake na wakati mwingine anaweza hata kupata mayai kutoka kwa mwanamke mwingine.

Namukwaya anakuwa mwanamke wa 25 nchini Uganda ambaye amezidi miaka 50 kupata mtoto kupitia mfumo wa IVF, kwa mujibu wa Dkt Ssali.

Dkt Herbert Kalema, mtaalamu wa masuala ya uzazi katika hospitali ya Masaka anasema wakati ambao Namukwaya aliporipotiwa kufika hospitalini hapo wiki tatu zilizopita alikuwa na maumivu, mapigo ya moyo yanaenda kasi na alikuwa anapata wakati mgumu kupumua na kutokwa jasho kwenye miguu.

"Tulikuwa tunafahamu vizuri historia yake wakati mama huyo alipowasili hospitalini akiwa na miezi nane, hatukutaka ajifungue kawaida ndio maana tulitaka kumfanyia upasuaji. Tunamshukuru Mungu kila kitu kilienda sawa,"alisema.

Alisema baada ya oparesheni, Namukwaya akawa mwenye nguvu na kuanza kumnyonyesha mtoto wake.

Mtoto alizaliwa akiwa na uzito wa kawaida wa kilo 2.6, alisema Dkt Kalema.

"Huyu ni mwanamke wa hamsini ambaye ana umri zaidi ya miaka hamsini kujifungua kwa oparesheni na kila kitu kwenda salama," alisema.

Dkt Kalema alisema Namukwaya alihudhuria kliniki katika kituo cha Women's Hospital International and Fertility Centre, lakini wakati wa marufuku ya kutoka nje kuzuia maambukizi ya corona ilimbidi ahamie hospitali ya Masaka.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO