Al Shabaab wavamia kambi ya polisi, Garissa

Kamishana wa kanda ya Kaskazini Mohamed Birik kushoto na Kaunti Kamishma wa Garissa Meru Mwangi
Kamishana wa kanda ya Kaskazini Mohamed Birik kushoto na Kaunti Kamishma wa Garissa Meru Mwangi
Jumamosi usiku Wapiganaji wa kundi la Al Shabaab walishambulia kutuo kimoja cha polisi wa kushika doria mpakani katika eneo la Yumbis, Kaunti ndogo ya Fafi katika kaunti ya Garissa, kilomita 90 kutoka mpaka wa Kenya na Somalia.

Inasemekana wanamgambo hao waliteketeza kituo hicho huku ripoti za awali zikidai kuwa walitoweka na bunduki kadhaa na silaha zinginezo.

Wanasema wavamizi hao walionekana kufahamu eneo hilo vyema. Huku wengine wakifyatua risasi wenzao walikuwa wakiharibu mnara wa mawasiliano wa Safaricom na wengine wakiwasha moto kambi hiyo. Shambulizi hilo lilichukuwa muda wa dakika 30.

Polisi wote 20 walikuwa katika kambi hiyo wako salama huku idara ya polisi ikisema kwamba wapiganaji wawili waliuawa wakati wa makabiliano hayo.

Uvamizi huo unajiri wiki moja tu baada ya maafisa saba wa polisi kuuawa wakati gari walimokuwa wakisafiria lilipokanyaga kilipuzi cha kufichwa ardhini.