Al Shabaab wavamia kambi ya polisi ya Dajabula

Wavamizi wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabaab walivamia kambi ya polisi ya Dajabula katika Kaunti ya Wajir Jumanne usiku.

Kulingana na afisa msimamizi wa kituo hicho, Stapol Habaswein, tukio hilo lilitokea kilomita 13 kutoka mpaka wa Kenya na Somalia.

Kamanda wa polisi Simon Areba ambaye alikuwa miongoni mwa maafisa wa usalama waliokuwa wakishika doria alisema kwamba walivamiwa wakati mvua ilipokuwa ikinyesha na giza totoro.

Maafisa walisikia mlio wa risasi za wavamizi waliokuwa wakipiga kelele katika lugha ya kisomali na wakalazimika kutawanyika ili kujificha na kupanga mikakati ya kujibu mashambulizi.

"Kulikuwa na giza na maafisa wakatawanyika kwenda pande tofauti kutoka kambi hiyo na makabiliano kuanza,? kamanda alisema.

Alisema alikimbia umbali wa takriban mita 200 kujificha. Hajarejea kambini lakini amekuwa akiwasiliana kupitia simu yake ya mkononi. Maafisa wa KDF kutoka kambi ya Dajabula wametumwa kuwasaka wavamizi hao.

Idadi ya waliofariki au kujeruhiwa kutokana na shambuliz hilo bado haijatolewa. Afisa mkuu wa polisi wa kituo hicho Stapol Habaswein amesema ripoti kamili itatolewa baada ya maafisa husika kukamilisha uchunguzi wao.