‘Alichagua maid na akaniacha nijilipie nyumba.’ Mwanamke asimulia kuachwa na mumewe aliyetoroka na mfanyikazi wao wa nyumbani

Side view of young woman with eyes closed
Side view of young woman with eyes closed
Baada ya miaka saba  katika ndoa,  Caren  hakutarajia kwamba mumewe Mike  angemsaliti na kumuacha hoi kwa njia iliyomvunja moyo kabisa na kumkosesha imani kwa jina ‘mapenzi’.

Yota  yalianza  baada ya Caren kujifugua mtoto wao wa pili  na akaanza kugundua kwamba palianza kuwepo pengo la  mawasiliano  kati yake na mumewe. Caren alisononeshwa na  mtindo wa kuwepo ugomvi kila mara wakati yeye na Mike walipokuwa wakizungumza. Uhusiano wao ulivurugika kabisa na wakati mwingi Mike angelala sebuleni  pindi tu tofauti kati yao ingeibuka .

Caren alijaribu kadri ya uwezo wake kumaliza tofauti za kila mara na mume wake lakini Mike yaonekana alikuwa na  makovu mengi dhidi ya mkewe na isitoshe hakuwa tayari kuyazungumzia ili kuinasua ndoa yake. Alianza kugundua kwamba  Mike wakati mwingi alikuwa hazungumzi naye lakini akija nyumbani angempata akitabasamu sana huku akichekeshwa na mfanyikazi wao wa nyumbani.

‘Tungegombana asubuhi kwa mfano na ningetoka ili nisizidishe malumbano ,baadaye nikija nyumbani ,ningempata Mike akichekeshwa  kwa  kiasi cha kutokwa machozi wakati anapopiga gumzo na mfanyikazi wetu wa nyumbani’ anasema Caren .

Kwa  muda, pia Caren aligundua kwamba mfanyikazi wao yule alikuwa ameanza kumfanyia kiburi. Caren hakuweza kumfurusha wakati ule kwa sababu alihitaji mfanyikazi ambaye amezoeana na watoto wake alipokuwa akienda kazini. Alijiambia kwamba wakati utakapofika, angemtimua yule mfanyikazi kwani alianza kugundua kwamba mfanyikazi wao wa nyumbani alikuwa akizidisha chumvi kujenga uhasama kati yake na mume wake Mike.

Ulimwengu wa Caren hata hivyo ulimgeuka siku moja alipoamua kwamba ameyapitia ya kutosha  na kuamua kumfungisha virago yule mfanyikazi. Alipogundua kilichotokea, Mike alihamakishwa sana na hatua ya mkewe kumfurusha yule mfanyikazi. Alihoji hatua ya mkewe kumfukuza mfanyikazi yule pia kushauriana naye kwanza licha ya kwamba ni Caren ndiye aliyemtafuta mfanyikazi huyo na hata aliwajua jamaa zake. Caren alithibitisha alichokuwa akiambiwa na majirani kwamba mume wake alikuwa amejenga uhusiano wa karibu sana na  mfanyikazi wao kwa kiwango cha kuwahofisha rafiki wengi wa Caren .

‘ Rafiki zangu wengi walikuwa wakinionya kwamba mfanyikazi wangu wa nyumbani angenipokonya mume, lakini nilipuuza hilo kwani sikufahamu kwamba tofauti kati yangu na Mike zilikuwa zikimpeleka karibu na msichana huyo.’ Anasema Caren .

Wiki mbili baada ya Caren kumfukuza yule  mfanyikazi wa nyumbani, Mike alibeba nguo zake na kumuacha Caren na watoto kisha akaelekea zake kuanza maisha na  mfanyikazi wao  wa nyumbani. Caren  aliachwa kinywa wazi asijue cha kufanya. Jamii pia haikumrahisishia kazi kwani wengi walifanyia kejeli kwamba kapokonywa mume na mfanyikazi wake. Ilikuwa njia ngumu na yenye machungu sana kwa Caren kujua kweli  kwamba kikulacho kweli ki nguoni mwako .