logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Nimeona viwanja bora Afrika!" Larry Madowo akejeli uwanja wa Man United juu ya paa inayovuja

"Kama singerekodi maporomoko ya maji ya Old Trafford mwenyewe, nisingeamini," Madowo alisema.

image
na SAMUEL MAINA

Burudani13 May 2024 - 08:06

Muhtasari


  • •Madowo alirekodi baadhi ya matukio muhimu ya mechi hiyo na kuchapisha picha na video kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii.
  • •"Kama singerekodi maporomoko ya maji ya Old Trafford mwenyewe, nisingeamini. Nimeona uwanja mzuri zaidi barani Afrika,” alisema.

Mwanahabari maarufu wa kimataifa wa Kenya Larry Madowo alikuwa miongoni mwa maelfu ya mashabiki wa soka waliotazama moja kwa moja mechi ya Manchester United dhidi ya Arsenal kwenye uwanja wa Old Trafford siku ya Jumapili jioni.

Mwandishi huyo wa habari wa CNN ambaye anashabikia Arsenal alifurahia kutazama moja kwa moja huku klabu yake anayoipenda zaidi ikishinda 0-1 dhidi ya wapinzani wao wa muda mrefu katika mechi iliyojaa hisia kemkem.

Madowo alirekodi baadhi ya matukio muhimu ya mechi hiyo na kuchapisha picha na video kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii.

“Je, ninunue tiketi ya mchezo wa leo? Au Arsenal watanivunja moyo, na nihifadhi pesa zangu?” Larry Madowo aliandika kwenye Twitter kabla ya mchezo huo.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha ya nje ya uwanja wa Old Trafford.

Wakati mechi ikiendelea, mwanahabari huyo mahiri aliwasasisha wafuasi wake na kuwafahamisha kwamba alikuwa amekaa pamoja na mashabiki wa Manchester United hivyo haikuwa rahisi kwake kusherehekea mabao ya Arsenal.

"Nadhani Arsenal wanashinda mchezo huu," aliandika wakati mechi ikiendelea.

Pia alionekana kusherehekea baada ya mechi kumalizika huku wanabunduki wakiwa mbele kwa 0-1.

Kando na matukio ya mchuano huo, mwanahabari huyo wa zamani wa KTN na NTV pia alibaini uvujaji mkubwa kwenye paa la Old Trafford ambao ulifanya maji mengi kumwagika kwenye sehemu ambapo mashabiki hukaa.

"Mvua kubwa Old Trafford lakini mashabiki wa Arsenal hawajaacha kuimba. Ushindi ulioje!” aliandika chini ya video ya mvua kubwa kunyesha katika uwanja huo.

"Paa ya Man United inavuja kama safu yao ya ulinzi!" Madowo alilalamika.

Chini ya video nyingine ya uvujaji mkubwa kwenye paa la uwanja huo, Madowo alionekana kudai kuwa uwanja huo ulikuwa katika hali mbaya zaidi kuliko baadhi ya viwanja barani Afrika.

"Kama singerekodi maporomoko ya maji ya Old Trafford mwenyewe, nisingeamini. Nimeona uwanja mzuri zaidi barani Afrika,” alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved