In Summary

•Bradley alimtembelea mzazi huyu wake katika eneo la Chavakali kaunti ya Vihiga wikendi akiandamana na wasimamizi wake.

•Mamake Bradley alishindwa kuficha furaha yake huku akimsalimia mwanae na kumkaribisha nyumbani.

Bradley Marongo na mamake
Image: HISANI

Furaha ilitanda hewani huku kijana mrefu maarufu Bradley Marongo almaarufu Gen z Goliath akiungana na mama yake kwa mara ya kwanza tangu apate umaarufu.

Bradley ambaye kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja uliopita amekuwa akizuru nchi na kufanya madili makubwa alimtembelea mzazi huyu wake katika eneo la Chavakali kaunti ya Vihiga wikendi akiandamana na wasimamizi wake.

Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, alichapisha video iliyomuonyesha akimkumbatia mamake kwa furaha baada ya kuwasili nyumbani. Mzazi huyo alishindwa kuficha furaha yake huku akimsalimia mwanae na kumkaribisha nyumbani.

"Nilisafiri 378Km kukutana na mama yangu," Bradley alisema.

Kijana huyo mrefu ambaye alipata umaarufu wakati wa maandamano ya Gen z alionekana kufurahishwa sana kurudi nyumbani na ilionekana wazi kwenye video na picha zilizoshirikiwa.

Katika video moja, alionekana akipakua baadhi ya vitu vizuri alivyokuwa ameenda nazo nyumbani kwa wazazi wake na katika video nyingine alionekana akila chakula kilichoandaliwa na mama yake.

"Mashariki au Magharibi, nyumba ni bora," alisema.

Ziara ya wikendi inaaminika kuwa mara ya kwanza Bradley anazuru nyumbani tangu alipopata umaarufu takriban miezi miwili iliyopita.

Mapema mwezi huu, mama huyo alijitokeza kwenye mahojiano ambapo alimshutumu kwa kumtelekeza tangu alipopata umaarufu na kumtaka amkumbuke.

Alihojiwa na kukiri kwamba mwanawe aliacha kuchukua simu zake tangu umaarufu kumjia mwezi mmoja uliopita.

"Bradley hata sahii nikipiga simu hashikii..wale manager ako wao wawili wamemshika..si rahisi anipigie simu..nilikuwa Nairobi, wakati mtoto alitoka Mombasa mara ya kwanza, hakuna siku alikanyaga mahali naishi," mamake Bradley alisema.

Bradley hata hivyo baadaye alisisitiza kwamba madai ya mama yake kwamba tangu apate umaarufu aliitelekeza familia yake ni uongo.

Akijibu madai hayo, kijana huyo mrefu alisema kwamba yeye huwapigia simu na hata kuwatumia hela za matumizi.

Alidai kwamba shida kuu ya mama yake ni kutaka asafiri naye kila mahali anapokwenda, akitolea mfano ziara ya hivi majuzi kuenda Pwani kwa ndege.

“Huwa nawatumia pesa na hata [mama] akitoka Nairobi nilimpa pesa na bado huwa nawatumia. Shida ya mama yangu anataka nikienda mahali kamaMombasaeti niende na yeye, na hilo halitowezekana, Bradley alisema.

Kuhusu mwanamke anayedaiwa kuwa mke wake, Bradley alisema kuwa alimtoroka wakati hakuwa na pesa na sasa anataka kurudi kwa kujilazimisha kwake baada ya kuona nyota yake imeangaza tena.

"Ako, lakini sasa shida ya huyo msichana vile sikuwa na doh, akaamua kutoroka na vile tuliachana na yeye alienda kuoleka kwingine...sahii vile nimeanza kushika elfu tatu, nne, tano hivi, amesema sisaidii mtoto..na ashaolewa" aliongeza.

View Comments