In Summary

•Video inayoonyesha mwanamume akimuombea Bradley huku wanafamilia wengine na watumishi wa kanisa wakijiunga na maombi.

•Bradley alipata fursa ya kuwa karibu na mama yake kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu tangu kupata umaarufu.

Image: FACEBOOK// BRADLEY MTALL GEN-Z GOLIATH

Maombi maalum yalifanywa kwa ajili ya kijana mrefu maarufu Bradley Marongo almaarufu Gen-z Goliath kufuatia kurejea nyumbani wikendi ambayo imepita.

Kijana huyo ambaye alipata umaarufu wakati wa maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen-z alichapisha video inayoonyesha mwanamume akimuombea huku wanafamilia wengine na watumishi wa kanisa wakijiunga na maombi.

Katika video hiyo, Bradley anaonekana akiwa amepiga magoti huku mwanamume huyo akitoa maneno ya shukrani na baraka juu yake.

“Asante kwa sababu ya kijana nyumbani. Mungu unaporejesha Watoto nyumbani, sisi kama jamii na familia tunainua jina lako. Tunaomba Watoto wasije kupotelea mjini. Muonekanie kijana, mguse kijana. Asante kwa kumzingira, asante kwa kumkumbuka..” alisikika mwanaume huyo akimuombea Bradley akiomba.

Bradley alirejea nyumbani mwishoni wikendi na kupata fursa ya kuwa karibu na mama yake kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.

Furaha ilitanda hewani wikendi huku kijana huyo mrefu akiungana na mama yake kwa mara ya kwanza tangu apate umaarufu.

Bradley ambaye kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja uliopita amekuwa akizuru nchi na kufanya madili makubwa alimtembelea mzazi huyu wake katika eneo la Chavakali kaunti ya Vihiga wikendi akiandamana na wasimamizi wake.

Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, alichapisha video iliyomuonyesha akimkumbatia mamake kwa furaha baada ya kuwasili nyumbani. Mzazi huyo alishindwa kuficha furaha yake huku akimsalimia mwanae na kumkaribisha nyumbani.

"Nilisafiri 378Km kukutana na mama yangu," Bradley alisema.

Kijana huyo  alionekana kufurahishwa sana kurudi nyumbani na ilionekana wazi kwenye video na picha zilizoshirikiwa.

Katika video moja, alionekana akipakua baadhi ya vitu vizuri alivyokuwa ameenda nazo nyumbani kwa wazazi wake na katika video nyingine alionekana akila chakula kilichoandaliwa na mama yake.

"Mashariki au Magharibi, nyumba ni bora," alisema.

Ziara ya wikendi inaaminika kuwa mara ya kwanza Bradley anazuru nyumbani tangu alipopata umaarufu takriban miezi miwili iliyopita.

Mapema mwezi huu, mama huyo alijitokeza kwenye mahojiano ambapo alimshutumu kwa kumtelekeza tangu alipopata umaarufu na kumtaka amkumbuke.

View Comments