In Summary

•Marite alitoa shukrani zake kwa mwimbaji huyo wa nyimbo za Kikuyu kwa nafasi aliyompa kuhudumu.

•Aliendelea kuomba radhi kwa makosa ambayo huenda aliyafanya alipokuwa akitekeleza majukumu yake.

Marite na Samidoh
Image: HISANI

Moses Marite, meneja wa zamani wa staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh ametoa taarifa kufuatia matukio ya hivi majuzi ambapo aliachishwa kazi.

Katika taarifa ambayo alichapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Marite alitoa shukrani zake kwa mwimbaji huyo wa nyimbo za Kikuyu kwa nafasi aliyompa kuhudumu.

Meneja huyo wa muziki aliitaja fursa hiyo kuwa zawadi kubwa na akaeleza kuwa anathamini sapoti ambayo msanii huyo amempa

"Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Samidoh kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuwa sehemu ya bendi yake kubwa. Kila fursa ya kuhudumu ni zawadi, asante kwa kuniruhusu nifungue na wewe, " Marite alisema kupitia mtandao wa Facebook.

Aliendelea kuomba radhi kwa makosa ambayo huenda aliyafanya alipokuwa akitekeleza majukumu yake.

"Usaidizi wako umekuwa mkubwa sana.. Kupitia wewe, nimefanikisha mengi ambayo yanaweza kuhusishwa na wewe tu. Ninaomba msamaha wa dhati kwako kwa matukio ambayo nimekukosea wewe na chapa yako kwa kujua na bila kujua nilipokuwa nikitekeleza majukumu yangu," Alisema.

Marite alibainisha kuwa safari yake na nyota huyo wa Mugithi imekuwa na panda shuka nyingi.

Aidha, pia alifichua kuwa alijitengenezea marafiki wengi wakubwa katika safari hiyo na pia akatoa shukrani zake kwa mashabiki kwa sapoti yao.

"Mabadiliko ya maisha hayaepukiki, nimefikia dari. Kwa hiyo naitakia chapa/bendi hii kila la kheri na ninaamini bila shaka itaendelea kuimarika kama ilivyokuwa siku zote, asante kwa mara nyingine na Mungu mwema, abariki kila mmoja wenu,” alisema.

Samidoh alitangaza kuachishwa kazi kwa meneja wake Marite mapema wiki hii akiweka wazi kuwa haruhusiwi tena kufanya makubaliano yoyote kwa niaba yake.

Sababu ya hatua hiyo ya kushangaza hata hivyo haikuwekwa wazi na mashabiki wameachwa tu kukisia.

View Comments