In Summary

• Arsenal walimenyana na Manchester City jioni ya Jumapili katika uga wa Etihad ambapo mechi hiyo iliishia kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

• Arsenal walilazimika kucheza kipindi cha pili chote wakiwa 10 uwanjani baada ya kadi nyekundu kwa Trossard.

KAREN NYAMU
Image: FACEBOOK

Seneta maalum Karen Nyamu amemuomba Mungu kuwapa ufunuo wa kipekee mashabiki wa Arsenal, haswa kutoka nchini Kenya, ukiwa ni msimu wa tatu ambapo wanachukuliwa kuwa wawaniaji wa ubingwa wa ligi baada ya kuponyokwa kwa ukareibu mara mbili.

Nyamu ambaye pia ni shabiki wa Arsenal, alitoa ujumbe huo kwa Mungu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii akisema kwamba safari hii wao kama wanabunduki wanatumai wataibuka na ubingwa wa ligi kuu ya EPL.

Hata hivyo, Nyamu alimuomba Mungu kuwapa ufunuo mashabiki ili kujua mapema kama kweli klabu yao ni kama Musa kutoka simulizi za Biblia anayesemekana kuiona nchi ya ahadi – Kaanani- lakini akafa bila kutia guu lake kule.

Hii ni sawa na Arsenal ambao katika misimu miwili iliyopita, wamekuwa wakikaribia kutwaa ubingwa wa EPL lakini ubingwa huo unawatoka wakati wa kipindi cha lala salama kwenye msimamo wa ligi hiyo ya Uingereza inayoshabikiwa zaidi humu nchini.

“Saa hii ndio nguvu ya ku watch EPL inarudi. Nimepona msimu uliopita. Mungu kama Arsenal ni Musa ambaye aliona lakini hajawahi kufika nchi ya ahadi utwambie,” Nyamu alisema.

Arsenal walimenyana na Manchester City jioni ya Jumapili katika uga wa Etihad ambapo mechi hiyo iliishia kwa sare ya kufungana mabao 2-2, Arsenal wakilazimika kucheza kipindi cha pili chote wakiwa 10 uwanjani baada ya kadi nyekundu kwa Trossard.

View Comments