In Summary

• Baadae, alisasisha ujumbe akisema jinsi Wakenya walimsherehekea si tu kwa maneno matupu mitandaoni lakini pia kupitia mtandao wa kutuma pesa wa M-Pesa.

• Alisema kwamba alipokea jumbe nyingi za M-Pesa kutoka kwa watu wanaofurahia kazi yake mitandaoni na kufichua nini atakachofanya na pesa hizo.

KEBASO.
Image: FACEBOOK

Mwanaharakati wa kutoa elimu ya kiraia kwa Wakenya mitandaoni, Morara Kebaso Snr amepokea mamia ya jumbe za salamu za heri njema leo hii anaposherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Mapema, Kebaso alifichua kwamba alikuwa anatarajia siku yake ya kuzaliwa iwe nzuri, akiweka wazi kwamba alikuwa anafikisha umri wa miaka 29.

Baadae, alisasisha ujumbe akisema jinsi Wakenya walimsherehekea si tu kwa maneno matupu mitandaoni lakini pia kupitia mtandao wa kutuma pesa wa M-Pesa.

Alisema kwamba alipokea jumbe nyingi za M-Pesa kutoka kwa watu wanaofurahia kazi yake mitandaoni na kufichua nini atakachofanya na pesa hizo.

“Nimepokea jumbe nyingi sana za mpesa tangu asubuhi. Hii itakuwa siku yangu ya kuzaliwa bora tangu nilipozaliwa. Siwezi kutuma ujumbe wa ‘asante’ kwenu nyote ila ASANTENI SANA,” alisema.

Kwa mujibu wa Kebaso, hela hizo alizotumiwa kusherehekea miaka yake 29 ya kuzaliwa hatozitumia kwenye sherehe bali atatumia kununua vyombo vya kisasa kwa ajili ya kuendeleza harakati za kuelimisha wananchi.

“Sitatumia zawadi hizo kwa sherehe badala yake nitatumia pesa hizo kununua vifaa vya studio ya utangazaji mtandaoni katika moja ya vyumba vyetu ambavyo vitakuwa vikiendesha mazungumzo ya elimu ya uraia katika lugha za kienyeji,” alisema.

Kebaso amekuwa kero kwa wengi haswa wale walioko serikalini kutokana na harakati zake za kutembea kote nchini akionyesha hali ya kutamausha ya miradi ambayo ilizinduliwa siku nyingi zilizopita bila kutekelezwa.

Hivi majuzi, alipokea gari la kufanyia ziara hizo na kutumia michango aliyochangiwa kununua vyombo vya sauti.

Wiki iliyopita pia Morara alionyesha jumba la kifahari katika mtaa wa Kahawa jijini Nairobi ambalo alidai alipatiwa kama zawadi na mtu anayefurahia kazi anayoifanya ya kuwatoa taka maskioni Wakenya.

View Comments