In Summary

• Stevo Simple Boy ameachia wimbo mapema Alhamisi akitumia utunzi wake kueleza maana ya kauli hiyo ambayo pia ameitumia kama kichwa cha wimbo wake.

• Mapema mwezi huu akiwa katika runinga moja humu nchini, Stevo alifichua kwamba mwezi ujao anatarajia kusafiri kwenda nchini Saudia kwa ziara ya kikazi.

Stevo Simple Boy.
Image: HISANI

Msanii mwenye utata, Stevo Simple Boy amepiga hatua zaidi katika kuelewesha mashabiki wake kuhusu kauli aliyodai kuwa ilimshindia ziara kwenda kutumbuiza nchini Saudi Arabia – Mafi mafi mushkila.

Stevo Simple Boy ameachia wimbo mapema Alhamisi akitumia utunzi wake kueleza maana ya kauli hiyo ambayo pia ameitumia kama kichwa cha wimbo wake.

“Mafi, mafi….mafi, mafi mafi, mushkila…yente yente mambo iko sawa, hakuna matata, vile niko simple (hakuna matata) sihitaji kadimple (hakuna matata) acha leo nivunje shingo, nikiserereka…” baadhi ya mistari kwenye wimbo huo inaimba.

Mapema mwezi huu akiwa katika runinga moja humu nchini, Stevo alifichua kwamba mwezi ujao anatarajia kusafiri kwenda nchini Saudia kwa ziara ya kikazi.

Alieleza kwamba alishinda ziara hiyo ambayo itakuwa yake ya kwanza maishani kusafiri nje ya mipaka ya Kenya, shukrani kwa kauli hiyo.

“Kwa nini mimi kila mara ninabadilisha muonekano wa nywele, mavazi na pia misamiati? Unajua mimi ni msanii si Kenya peke yake, ni Afrika Mashariki nzima lakini sasa nataka kutanua mbawa zaidi niende kimataifa,” Stevo alifafanua.

“Kwa hiyo mefi mefi muskla ni lugha ya Kiarabu, wakati nilisema hivyo, unajua nini kilifanyika? Ni bahati tu ilinitokea, mwezi ujao ninaenda Saudi Arabia kwa kusema tu ‘mefi mefi muskla’. Tarehe 23 Septemba nitakuwa napiga shoo Riyadh,” Stevo alifafanua zaidi.

View Comments