In Summary

• Kwa kipindi cha wiki moja iliyopita, amekuwa akipapurana na mwanasosholaiti Huddah Monroe lakini sasa ugomvi wake umeonekana kuhamisha mishale na kumlenga YouTuber Andrew Kibe

SALASYA NA KIBE
Image: HISANI

Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya katika siku za hivi karibuni ameonekana kujijengea maadui wengi kuliko marafiki katika mitandao ya kijamii.

Kwa kipindi cha wiki moja iliyopita, amekuwa akipapurana na mwanasosholaiti Huddah Monroe lakini sasa ugomvi wake umeonekana kuhamisha mishale na kumlenga YouTuber Andrew Kibe.

 Inaarifiwa kwamba Kibe na Salasya walianza kushambuliana kwenye mtandao wa Instagram Alhamisi baada ya YouTuber huyo mwenye ulimi wa moto kufanya video akimkashifu Salasya kwa tabia zake ‘za kienyeji’ licha ya kuwa mtu anayestahili kuheshimiwa katika jamii.

Salasya akimjibu, aliandika aya ndefu akimzomea Kibe kwamba yeye anayemuona kama mpumbavu tayari ashakuwa mbunge huku pia akijinadi kwamba utajiri wake ni maradufu zaidi ya ule wa Kibe.

“Haijalishi utafanya video ngapi kwenye YouTube yako ukiambia dunia jinsi mimi ni chizi wa ushago kana kwamba wewe utakapokufa utazikwa Nairobi CBD ama Tom Mboya Street, venye nacheka kifalafala sijui kienyeji as if wewe ndio broiler, kamwe haitabadilishe maisha yako,” Salasya alimchoma Kibe mkuki.

“Nataka nikukumbushe kuwa hautawahi kuwa mbunge maishani mwako na mimi Fala ni tajiri kuliko wewe,” aliongeza.

Mbunge huyo alitishia kumkaba Kibe hata zaidi, akisema kwamba hatokaa kimnyonge na kuona jina lake likipakwa tope na YouTuber huyo mwenye hulka za kuwashambulia watu kwa kauli na maneno hasi.

“Sasa nitaacha upuuzi wako. Umetusi watoto wa wenyewe kwa muda mrefu kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kukushughulikia sasa twende, kumbuke mimi ni mwanasiasa hana cha kupoteza katika upuuzi huu wa mtandaoni. Nipo kwenye mitandao ya kijamii tu kwa ajili ya kujifurahisha. Watu wangu hawajali kuhusu mambo ya mitandaoni bali kile ninachowafanyia, Mimi ni mtu ambaye nimepitia mitihani yote ya maisha,” Salasya alitema moto.

Kujibizana huku kunajiri siku chache tu baada ya Salasya kumuomba Kibe msamaha kwa kile alidai ni kukosa kufuata ushauri wake kumhusu mwanadada Huddah Monroe.

Kibe alisema kwamba kuanzia sasa atamheshimu Kibe kama mtu aliyetangulia kuliona jua mbele yake.

View Comments