In Summary

•Porter aliweka historia kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal.

•Josh Nichols (18), Jack Porter (16), Ethan Nwaneri (17), Myles Lewis-Skelly (18), Maldini Kacurri (18) na Ismael Kabia (18) pia walicheza.

Jack Porter aliwakilisha Arsenal kwenye mchuano dhidi ya Bolton Wanderers
Image: HISANI

Kocha wa Arsenal Mikel Arteta aliweka wazi kwamba hakuwa na chaguo bora zaidi ila kumchezesha kipa Jack Porter mwenye umri wa miaka 16 wakati wa pambano lao dhidi ya Bolton Wanderers kwenye mchuano wa Carabao Cup mnamo Jumatano jioni.

Porter aliweka historia kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal katika mchezo wa kitaaluma. Ana miaka 16 na siku 72.

Katika mahojiano kabla ya mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Emirates, Arteta alisema kuwa makipa wake watatu bora na wenye uzoefu zaidi hawakuwa katika nafasi ya kucheza mchuano huo.

"Tuna David (Raya)akiwa na jeraha, Neto amefungiwa kucheza katika kombe hili na Tommy (Setford) ameumia kwa bahati mbaya, kwa hivyo inabidi kumchezesha (Porter)," Arteta aliwaambia waandishi wa habari.

Aliongeza kuwa mchezo huo ulitoa fursa nzuri kwa kijana huyo wa miaka 16 na kusifu tabia yake.

“Ni fursa iliyoje kwake! Yeye ni mhusika mzuri. Anafanya mazoezi nasi kila siku, kwa hivyo amezoea,” kocha huyo alisema.

Arteta alitoa fursa kwa wachezaji kadhaa chipukizi kwenye mechi ya Kombe la Carabao dhidi ya Bolton Wanderers inayocheza kwenye League One.

Wachezaji wanne walio chini ya umri wa miaka 20 walihusika kwenye kikosi cha kwanza huku wengine wawili wakihusishwa baadaye kwenye mechi hiyo.

Wachezaji chipukizi waliohusishwa ni pamoja na Josh Nichols (18), Jack Porter (16), Ethan Nwaneri (17), Myles Lewis-Skelly (18), Maldini Kacurri (18) na Ismael Kabia (18).

Kocha Arteta aliwasifu vijana hao na kubainisha kuwa walikuwa na imani kubwa kuhusika katika mechi hiyo muhimu huku Wanabunduki wakitarajia kusonga mbele kwa hatua inayofuata ya Kombe la Carabao.

View Comments