In Summary

•Pamela alipopigiwa simu, alithibitisha kwamba amekuwa akimshuku mumewe kuwa na mipango wa kando.

•"Kama kuna mke ananimezea mate, nataka nikuonye mimi ni mume wa wenyewe. Sitaki maneno yenu tena. Mwanamke yeyote akijaribu kunikaribia ni criminal offense," Mike aliapa.

Gidi na Ghost Studioni
Image: RADIO JAMBO

Mike Ochillo Mukhwana (46) kutoka Trans Nzoia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Pamela Naliaka (38) ambaye alikosana naye miezi michache iliyopita.

Mike alisema ndoa yake ya mwaka mmoja iliingia doa wakati mkewe alipompata na mipango wa kando.

Alisema ingawa bado hawajaachana, mkewe amekuwa akimshuku kuwa na mipango wa kando.

"Hapa mambo haiendi kaka. Nimekuwa na uhusiano na mwanamke. Nilikuwa nimeoa hapo awali, niko na watoto watatu. Mtu ambaye niko naye sasa hivi sina watoto naye. Nimekaa naye mwaka mmoja. Mahali kumetokea shida ni kwamba nimekuwa na mpango wa kando. Nilipokuwa naye, akafanya tukakosana na huyu mke wa pili," Mike alisimulia.

Aliongeza, "Vile nilikosana na mke wangu, Ilibidi niachane na mipango ya kando nikarudi kwake nikaomba msamaha. Tunaishi lakini bado ni kama ananishuku. Nataka nimhakikishie kwamba sina mpango mwingine wa kando kwa sababu aliamua kunipenda. Sina mke mwingine, ni huyu pekee yake. Mke wangu wa kwanza aliaga 2019."

Pamela alipopigiwa simu, alithibitisha kwamba amekuwa akimshuku mumewe kuwa na mipango wa kando.

Aidha alifichua kwamba amewahi kupata dalili za mumewe kutokuwa mwaminifu katika ndoa yao.

"Nilikuwa namshuku kwa sababu hatujakuwa na uhusiano mzuri. Nikiangalia simu yake napata meseji za wasichana. Kuna mwingine alimwambia anampenda, alikuwa anaambia mwingine akuje amuandike kazi," Pamela alifunguka.

Huku akiomba msamaha, Mike alimwambia mkewe, "Nataka nikudhibitishie mbele ya mamilioni ya mashabiki wanaosikiliza, wewe ndiye mke wangu. Nitakupenda kwa hali na mali. Nataka unisamehe kwa yale nimekuwa nikifanya. Sitarudia haya maneno. Yale yote nilikuwa nikifanya nimeyatoa katika moyo wangu na sitarudi."

"Mimi tayari nimekusamehe. Mambo ya wanaume huwezi jua lakini. Anaweza sema amebadilika lakini akarudia," Pamela alimjibu.

Baada ya kuahidi kubadilika, Mike alilazimishwa na mtangazaji Gidi kula kiapo cha kutomcheat mkewe tena.

"Mimi Mike Ochillo Mukhwana kutoka Trans Nzoia,  Nataka niwatangazia kwamba, kuanzia dakika hii, Pamela ndiye mke wangu. Na kama kuna mke ananimezea mate, nataka nikuonye mimi ni mume wa wenyewe. Sitaki maneno yenu tena. Mwanamke yeyote akijaribu kunikaribia ni criminal offense. Pamela nakupenda sana my dear," Mike alisema.

Pamela alimwambia mumewe, "Leo anakula nyama. Mike unajua mimi nakupenda kutoka kitambo. Mimi ni wako."

Je, maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi.

View Comments