Arsenal wajikakamua na kuilaza Aston Villa, Liverpool wainyuka Chelsea

Arsenal
Arsenal
Arsenal mara mbili ilitoka nyuma na kuinyuka Aston Villa mabao 3-2 kupitia kwa free kick ya Pierre-Emerick Aubameyang's dakika sita kabla ya mechi kutamatika ugani Emirates jana.

Kulikua na kiwewe kwamba huenda msururu wa kutofunga mabao ungewaandama Gunners wakati John McGinn alipowapa Villa uongozi lakini bao la kwanza la Nicolas Pepe akiwa Gunners likawapa vijana wa Unai Emery matumaini.

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp anasema kikosi chake hakina haja ya kushindana na mfumo wa Manchester City klabu hizo mbili zinaposhindana kileleni mwa ligi ya Primia.

The Reds hawakua katika hali zuri ya mashambulizi jana huko Chelsea lakini wakapata ushindi wa mabao 2-1 na kutetea uongozi wao wa alama tano mbele ya City kileleni. Kikosi cha Pep Guardiola nacho kiliwarambisha sakafu Watford 8-0 jumamosi.

Meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer anasema atasalia na matumaini licha ya kikosi chake kupoteza kwa West Ham mabao 2-0 katika uga wa London na kuwawacha Red Devils na alama nane tu kutoka kwa mechi zao 6 za ufunguzi.

Kikosi cha Solskjaer kimeshinda mechi mbili tu kati ya 11 za ligi ya Primia walizocheza na hawana ushindi wowote wa ugenini tangu Februari. Mabao ya Andriy Yarmolenko na Aaron Cresswell yaliwapa The Hammers alama zote tatu jana.

Kiungo wa Manchester United Marcus Rashford atafanyiwa uchunguzi baada ya kupata jeraha walipocheza dhidi ya West Ham. Rashford alianguka kunako kipindi cha pili wakati United walipopoteza mabao 2-0 kabla ya Jesse Lingard kuchukua mahala pake.

Meneja Ole Gunnar Solskjaer tayari anamkosa Anthony Martial na Mason Greenwood, ambaye alikosa mechi ya jana akiwa na homa ya mafua, lakini anatumai watakuwa tayari kucheza hivi karibuni.

Kwingineko, bao la kichwa la Karim Benzema kunako kipindi cha pili liliwapa Real Madrid ushindi wa 1-0 dhidi ya Sevilla huku kikosi cha Zinedine Zidane kikisalia bila kushindwa katika La Liga.

Real, ambao walipoteza 3-0 kwa PSG katika mechi yao ya ufunguzi ya ligi ya mabingwa wiki iliyopita wamepanda hadi katika nafasi ya pili kwenye jedwali na kumuondolea shinikizo meneja wao.

Tukirejea nchini, Gor Mahia waliregelea njia za ushindi walipowanyuka KCB mabao 2-1 katika uwanja wa Kenyatta huko Machakos jana. Francis Afriyie na Lawrence Juma waliwafungia mabingwa hao wa ligi ambao walikua wamepoteza 4-2 kwa USM Algiers katika mechi ya ligi ya mabingwa ya CAF.

Western Stima nao waliwacharaza Posta Rangers 1-0 uwanjani humo humo awali.