Arsenal wakamilisha usajili wa Nicolas Pepe kwa kitita cha pauni milioni 72

Arsenal wamekamilisha usajili wa wing'a wa Ivory Coast Nicolas Pepe kutoka Lille kwa kitita cha pauni milioni 72, kwa mchezaji huyo wa miaka 24 anayeaminika kutia saini mkataba wa miaka mitano.

Pepe alikua na msimu mzuri na Lille, akifunga mabao 23 katika mechi 41. Arsenal wanaaminika kuwapiku Napoli kumsajili Pepe na kiungo huyo atavaa sare nambari 19 ugani Emirates.

Ni mchezaji wa nne kusajiliwa na Gunners msimu huu wa joto baada ya Dani Ceballos, Gabriel Martinelli na William Saliba.

Napoli wamejipanga na kitita cha Euro milioni 60 kwa ajili ya winga wa Crystal Palace na mchezaji wa kimataifa wa Ivory Coast Wilfried Zaha baada ya kumkosa Pepe.

Kwingineko Barcelona wanataka kumuuza Mbrazili Philippe Coutinho, lakini wanahofia kuwa kuwa hawajapata ofa yoyote kumhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27.

Ole Gunnar Solskjaer anasema Manchester United bado wanajitahidi kusajili wachezaji kabla ya msimu mpya kuanza na kuwa anafurahishwa na bishara ya uhamisho ya klabu hiyo.

United wamemsajili Daniel James na Aaron Wan-Bissaka msimu huu wa joto na wako katika majadiliano kumsajili kiungo wa Juventus Paulo Dybala na mlinzi wa Leicester Harry Maguire.

Tukisalia Uingereza, Tottenham wameanzisha majadiliano na Sporting Lisbon kwa ajili ya Bruno Fernandes. Wawakilishi wa Spurs walikutana na maafisa wa Sporting jijini Lisbon jana.

Majadiliano hayo yanaaminika kuwa ya awali lakini Fernandes anadhaniwa kuweza kuchukua nafasi ya kiungo wa kati wa Real Betis Giovani Lo Celso, ambaye amekuwa akiwaniwa na Mauricio Pochettino msimu huu wa joto.

Manchester United pia wanamtaka Fernandes lakini hajapewa kipa umbele na huenda mkataba wa Old Trafford usitokee.

Dirisha la uhamisho la la ligi ya Premier litafungwa Agosti tarehe 8.