Arsenal yalazwa na Brighton nyumbani na kuteremka hadi nafasi ya 10.

Masaibu ya Arsenal yalizidishwa siku ya Alhamisi walipolazwa nyumbani na Brighton katika mechi ya kwanza nyumbani kwa meneja wa muda Freddie Ljungberg.

Alexandre Lacazette aliadhimisha mechi yake ya 100 akichezea Arsenal kwa kusawazishia Gunnners bao baada ya Adam Webster kuweka wageni kifua mbele katika kipindi cha kwanza.

David Luiz alidhani ameipa Arsenal ushindi lakini bao lake lilikataliwa na VAR.

Arsenal sasa imesajili matokeo mabaya zaidi katika historia ya timu hiyo tangu mwaka 1977 huku wakiwa alama 10, nje ya nafasi ya kufuzu kwa dimba la ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Mwelekeo wa Arsenal ni upi kutoka hapa?

Arsenal ambao sasa wanashikilia nafasi ya 10 kwenye jadwali la ligi ya primia nchini Uingereza wamekosa kusajili ushindi katika mechi tisa zilizopita na mashabiki waliosalia uwanjani hadi mwisho wa mechi ya Alhamisi waliwazomea wachezaji baada ya mechi kukamilika.

Miaka 12 tangu mechi yake ya mwisho akichezea Arsenal Ljungberg alipewa fursa kuonyesha mashabiki wa timu hiyo kuwa anaweza kurejesha hadhi ya timu hiyo alipokuwa mchezaji.

Akiwa mchezaji alishinda mataji mawili ya Ligi ya Primia na mataji 3 ya FA.

Ljungberg alimtema Shkodran Mustafi kutoka kikosi chake cha wachezaji 18 dhidi ya Brighton baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Norwich wikendi iliyopita lakini hilo halikusaidia kwani safu yao ya ulinzi ilizidi kutapatapa na kuvuja hovyo.