Arsenali watoa ofa ya pauni milioni 40 kumsajili Wilfried Zaha

zaha
zaha
Arsenal wametoa ofa ya pauni milioni 40 kumsajili kiungo wa Crystal Palace Wilfried Zaha.

Mchezaji huyo wa umri wa miaka 26 amehusishwa sana na the Gunners msimu huu wa joto, ikiaminika kwamba anataka kusalia London na kucheza soka ya Uropa.

Hata hivyo huku ikiwa Palace tayari wamempoteza Aaron Wan-Bissaka kwa Manchester United kwa kitita cha pauni milioni 50, klabu hio haitaki kumuuza Zaha na wanamwekea thamani ya pauni milioni 80 maradufu ya ofa ya iliyowasilishwa na Arsenal.

Tukisalia Uingereza, Marcus Rashford ametia saini mkataba mpya wa miaka minne na Manchester United,  klabu hio ikiwa na chaguo la kuuongeza kwa mwaka mmoja zaidi na kumpeleka kupata kitita cha pauni elfu 200 kwa wiki.

Mchezaji huyo bora wa ligi ya Premier wa mwezi Januari mwaka huu amecheza mara kwa mara katika kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer tangu alipochukua uskani mwezi Disemba.

Amefunga mabao 50 na kusaidia mara 26 katika mechi 184, tangu alipochipuka katika kikosi cha kwanza mwaka wa 2016.

Kwingineko, Rafael Benitez amekubali kuwa meneja mpya wa klabu ya Uchina Dalian Yifang. Muhispania huyo huenda akazinduliwa kama meneja wa klabu hio hii leo kufuatia kujiuzulu kwa Choi Kang Hee.

Mkataba wa Benitez Newcastle ulitamatika jana na anatarajiwa kupata mshahara maradufu ya pauni milioni 6 aliyokua akipokea St James' Park. Meneja wa Porto Sergio Conceicao anasemekana kuitaka kazi Newcastle.