Askari wa kaunti ya Busia wapatikana na hatia ya kuwajeruhi wanahabari

Askari wawili wa serikali ya kaunti ya Busia Vincent Ngala na John Odongo wamepatikana na hatia na mahakama ya busia kwa tuhuma za kuwapiga na kuwajeruhi wanahabari wawili Frankline Bwire wa Royal Media na aliyekuwa mwanahabari wa ktn John Mondoh na kupewa kifungu cha nje cha miezi sita.

Kwenye uamuzi wake, hakimu wa mahakama hiyo, hakimu mkuu wa Busia Samson Temu amewapata wawili hao na hatia ya kuwapiga wanahabari hao katika afisi za gavana wa Busia Sospeter Ojaamong mnamo tarehe 15/7/2015 ingawa akawapa kifungu cha nje kwa vile hayo ndio makosa yao ya kwanza.

Wakili wa walalamishi Wycliffe Okuta amekaribisha uamuzi wa mahakama ingawa amedokeza kuwa wanalenga kuwasilisha kesi ya kudai fidia.

Waathiriwa Frankline Bwire wa Royal media na John Mondoh aliyekuwa katika runinga ya Ktn wamefurahishwa na uamuzi wa mahakama wakisema utakuwa funzo kwa wengine walio na mazoea ya kuwadhulumu waandishi wa habari.

Hata hivyo wakili wa washukiwa Joseph Makokha amesema wananuia kukata rufaa kutokana na uamuzi huo.