Askofu aliyetoweka na mke wa mtu auawa huko Juja

Askofu mmoja aliyetoroka na mke wa mtu mwaka jana ameuawa.

Mwili wa  Francis Mugweru, askofu wa kanisa la   Joyspring Soul Winning Worship church,  ulipatikana katika kichaka, mita 300 kutoka  boma lake la Kiganjo  huko Thika siku ya Ijumaa.

Mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 62  aligonga vichwa vya habari mwaka jana  Agosti  kwa kumpokonya muumini wake mmoja mkewe  pamoja na watoto wake watatu. Inaripotiwa alichukuliwa kwa lazima kutoka boma lake Alhamisi usiku  na kuigwa hadi kufa. Mwili wake ulikuwa na majeraha makubwa ya kukatwa  na kuna dalili za kupigwa na kifaa butu.

Kakake mhubiri huyo Samuel Njuguna amesema polisi wanafaa kuhakikisha kwamba waliotekeleza mauaji yake wanakamatwa na kushtakiwa.

“ Niliona mwili huo nilipokuwa nikienda kazini mjini Thika, saa moja baadaye nilipigiwa simu kuarifiwa kwamba  ni kakangu aliyekuwa ameuawa’

Kulingana na Njuguna,  mauaji hayo yalikuwa njama iliyopangwa vizuri  kwani waliotekeleza ukatili huo hawakuiba chochote na walichotaka ni uhai wake.

Katika kanisa la  Joy Spring Worship, waumini  wakiongozwa na kasisi   Lincoln Mwaniki,  walimtaja  mwendazake kama mpole na mtu aliyekuwa  na upendo .

“ Alikuwa mtu mzuri ambaye alitangamana vyema na watu ndio kwa sababu alifaulu kuanzisha makanisa ya kievangelisti katika eneo la Juja na sehemu zingine.’ Mwaniki alisema huku akizitaka mamlaka kuhakikisha kwamba haki inatendeka.

Mugweru  na mkewe  Agnes Wangivi  walitengana mwaka wa 2013 baada ya kuwa pamoja kwa miaka 34 na walikuwa na watoto watatu. Alikodisha nyumba katika eneo hilo na kuishi na mwanamke ambaye alikuwa amempokonya mmoja wa waumini wake, alikuwa mama ya watoto watano lakini wawili walibakia na baba yao.

 Kinaya ni kwamba Aksofu Mugweru  ndiye aliyesimamia harusi yao. Sahihi yake ipo katika cheti chao cha ndoa.

Askofu huyo alimshtumu mkewe kwa usinzi  na kwa kutishia kumuua  wakati alipoanza uhusiano na mke huyo wa mtu.

“ Aliuza gari letu na ng’ombe kadhaa ili kuendeleza tabia zake za usherati, pia nimekuwa nikiishi kwa hofu kwa sababu alitishia kuniua’ Askofu  Mugweru alidai wakati huo.

Mwili wake umehifadhiwa General Kago Funeral Home, Thika.