Athari za Corona! Muturi na Lusaka wasalimisha asilimia 30 ya mshahara wao

lusaka
lusaka
NA NICKSON TOSI

Spika wa bunge la kitaifa na Seneti Justin Muturi na Ken Lusaka, wametangaza kuwa watapunguza mishahara yao kwa asilimia 30 kwa miezi mitatu ijayo kama njia ya kusaidia serikali kuchanga hela za kukabiliana na mkurupuko wa virusi vya Corona.

Yanajiri haya siku moja tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kutangaza kuwa wameamua kupunguza mishahara yao kwa asilimia 80 kila mmoja.

Lusaka ambaye ni spika wa Seneti amesema wabunge wanashauriana kuhusiana na hatua hiyo na watakapoafikia hatua yao pamoja  watawafahamisha wakenya.

Muturi kwa upande wake anasema iwapo bunge la  kitaifa litaitisha vikao spesheli, basi wataweka mikakati maalum ili kuhakikisha kuwa wabunge hao hawaketi kwa ukaribu .

Lusaka ameongeza kuwa Seneti itarejelea vikao vyake juma lijalo akisema maseneta 15 kwa mujibu wa sheria za Seneti wanatosha kujadili miswada ya Seneti .

Yamkini kwa sasa takriban watu  472,000 kote ulimwenguni wanasemekana wako na virusi vya Corona, huku watu 114000 wakisemekana kuwa wamepona na wengine 21000 wakiwa wameaga dunia.

Utafiti huu umefanywa na chuo kikuu cha Johns Hopkins .