Athari za Covid-19 kwa vijana, maelfu waishi katika hali ya uchochole

Na Sairin Lupia

Huku taifa likiendelea kushuhudia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona, sekta nyingi za kiuchumi nchini na ulimwenguni zimeathirika sana, lakini kuna kundi moja la watu walioathirika pakubwa nchini. Vijana humu nchini wameathirika pakubwa sana. Kutoka kwa wale katika taasisi za elimu hadi mitaani wanaofanya kazi za jua kali.

Soma pia;

Takwimu zaonyesha kwamba nafasi nyingi za kazi zimepotea na wengi waliopoteza kazi zao ni vijana. Vijana wengi wa humu nchini wanatengemea kazi za vibarua kukidhi mahitaji yao ya msingi. Mikakati iliyotiwa na serikali kukabili kuenea kwa virusi vya corona imelemaza shughuli lnyingi za kibiashara.

Vijana wengi waliokuwa wamefungua biashara wamelazimika kuzifunga kwa sababu ya masharti yaliowekwa na serikali kudhibiti maambukizi ya corona; hamna wateja, saa za kuhudumu ni chache huku wengine wakihofia kuhangaishwa na polisi.

"Ili biashara inawiri unahitaji wateja na kama wateja wako hawana pesa basi hawatanunua bidhaa zako," alisema Barasa ambaye mmoja wa vijana waliofunga biashara zao mjini Nairobi.

Wengi wanasema kwamba kuna changamoto kubwa kupata wateja kwani wengi wao wamesalia manyumbani mwao kwa hofu ya maambukizi ya corona. Maelfu ya wafanyikazi katika sekta ya utalii na mahoteli ni vijana. Wengi wao waliachishwa kazi kwa sababu ya ukosefu wa wateja hasa kufuatia kufungwa kwa safari za ndege za kimataifa hali iliopelekwa kusitishwa kwa safari za watalii wanataka kuzuru taifa letu.

Wachuuzi katika jiji la Nairobi/ Maktaba

Changamoto hizi zimezaa shida bin shida miongoni mwa vijana, kwani walitegemea kazi hizi kujikimu. Wengi wamefurushwa kutoka nyumba zao za kukodi kwasababu wameshindwa kulipa kodi, swala hili limezua mjadala mkali nchini huku baadhi ya wananchi wakitaka serikali kuingilia kati ili kuwakinga wananchi wake dhidi ya dhulma za wenye nyumba wakatili.

Soma pia;

Ukosefu wa hela umefanya wengi wa vijana kugeukia kukopa. Kukopa miongini mwa vijana kumeongezeka mara dufu tangu kutua kwa janga hili. Hali hii imewatia vijana wengi mashakani hawana mahali pa kutoa hela za kulipia mikopo yao.

Waziri wa elimu George Magoha na mwanafunzi/ Maktaba

Waliovyuoni wamethirika pakubwa kwani shule zilifungwa tangia mwezi Machi na kulingana na waziri wa elimu George Magoha mwaka huu wa akademia umefutiliwa mbali. Hatua hii imewakera sana wanafunzi waliokuwa wanatarajia kumaliza masomo yao mwishoni mwa mwaka huu. Waziri siku ya Jumanne alitangaza kwamba shule zote zitafunguliwa Januari mwaka ujao na kwamba mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE haitafanyika mwaka huu, itafanywa mwaka ujao.

Sio kimasomo tu vijana pia wameathirika kisaikolojia na janga hili. Visa vya vijana kujitia kitanzi kwa sababu ya shida mbali mbali zimeongezeka, kwani janga hili limetia tu chumvi kwenye donda la shida za vijana. Huku shule zikisalia kufungwa visa vingi vya ulawiti na unajisi vimekuwa vikiripotiwa kila uchao. Mimba za mapema si habari geni sasa wasichana wengi wa umri mdogo wamepachikwa mimba.

Soma pia;

Uhuru azindua baluni za internet za loon ili kutumia vyema mtandao wa 4G

Lakini licha ya changamoto hizi pia kuna mwangaza. Tumeona ongezeko katika ubunifu miongoni mwa vijana huku wakitafuta vile wataishi. Wengi wametia bidii ya mchwa na kufanya kazi hapa na pale ilikusaidia wazazi. Katika muda huu pia vijana watumepata fursa ya kujifunza mengi na hata kuona vipaji walivyonavyo.

Kibinafsi sikuwa naandika kabla ya janga hili, lakini sasa nimepata kufahamu uwezo wangu kuandika makala kwa lugha ya Kiswahili, nashukuru Radio Jambo kwa kunipa fursa ya kuendeleza kipaji changu cha uandishi. Ingawa mengi yamefanyika ni  jukumu letu kama vijana kujikaza na kutumia vyema janga hili ili kuimarisha ubunifu wetu kujiendeleza.

Mwandishi ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO