Baada ya fungate Fred Arocho azidi kutalii mataifa tofauti (PICHA)

Zaidi ya miaka miwili iliyopita, tulikutangazia kuwa mtangazaji maarufu wa soka humu nchini, Fred Arocho, ndiye aliyesafiri zaidi ikilinganishwa na wenzake walio katika safu hiyo.

Kuongeza mchuzi kwa wali huu, ni kuwa hamna yeyote anayekaribia rekodi ya Arocho ya kusafiri duniani kote akiangazia mambo ya kispoti. Ameweza kuripoti na kuandika kuhusu michezo kama mashindano ya riadha, voliboli na pia soka.

Miongoni mwa mataifa na miji ambayo ameweza kutalii ni kama; Lesotho, Misri, Ureno, Uhispania, Ufaransa, Ubelgiji, Congo na pia Barcelona.

Hivi majuzi, Arocho alifunga safari hadi Ufaransa ambako alimpeleka mkewe, bi Sophie, akajivinjari katika fungate (honeymoon) yao ya pili miaka kumi tangu wawili hao walipo funga ndoa.

Akiwa humo Arocho ambaye pia alikuwa anafanya kazi za uanahabari, alishuhudia mechi za kirafiki za Harambee Stars dhidi ya Madagascar kabla ya kuelekea Uhispania kwa mechi nyingine dhidi ya DR Congo.

Baada ya mkewe kurudi nyumbani siku chache baadaye, bwana Laduuma sasa yumo Brussels, Ubelgiji ambapo pamoja na nduguye, Bill Arocho, wameelekea kuwatembelea marafiki zake ambao walicheza soka pamoja katika klabu ya KCB.

Baadaye, Arocho alisafiri hadi Amsterdam, mji mkuu wa Uholanzi ambapo alipata fursa ya kipekee ya kutembelea uwanja wa timu ya Ajax, ambao waliibuka kama mabingwa wa ligi kuu ya Eredivisie msimu uliopita.

Isitoshe, ziara za mtangazaji huyo wa Weekend warm up, bado hazijakamilika kwani atasafiri hadi mji wa Cairo, Misri kuungana na kikosi cha Harambee Stars.

Harambee Stars wapo Cairo kushiriki katika mashindano ya kombe la mataifa ya Africa (African cup of nations) ambayo yanaanza rasmi kesho.

Timu hiyo ya taifa itashiriki mechi yao ya kwanza Jumapili usiku dhidi ya Algeria, saa tano usiku saa za Afrika mashariki.