Baada ya kumtimua Duale ,Uhuru sasa anajitayarisha kulirekebisha baraza la mawaziri na ripoti ya BBI

Uhuru
Uhuru
Rais   Uhuru Kenyatta sasa anaweza kutangaza mabadiliko katika baraza la mawaziri na kuipokea ripoti ya BBI katika kipindi cha wiki mbili zijazo baada ya kufaulu kuwafurisha washirika wote wa naibu wake William Ruto kutoka nyadhifa za uongozi bungeni.

Katika mkutano uliodumu kwa dakika 22  wa  wabunge wa Jubilee, rais aliongoza kutimuliwa kwa Aden Duale kama kiongozi wa wengi bungeni na nafasi yake kuchukuliwa na mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya . Hatua  hiyo sasa inatoa fursa kwa rais Kenyatta kuweza kutangaza mageuzi katika baraza la mawaziri na pia kuhakikisha kwamba mapendekezo ya  jopo la BBI yanapitishwa bungeni bila vikwazo.

Ruto  amekuwa akipinga baadhi ya mapendekezo ya BBI huku washirika wake wakidai   kwamba mchakato huo mzima ulikuwa njama ya kumzuia kumrithi Kenyatta mwaka wa 2022. Duru zaarifu kwamba viongozi kadhaa wa upinzani na washirika wao watajumuishwa katika baraza jipya la mawaziri kando na kutengewa nafasi mbalimbali katika nyadhifa zingine kuu serikalini. Siku ya Jumatatu, Ruto alishuhudia  bila kuwa na uwezo wa kumsaidia  Mshirika wake Duale aliposalimishwa mbele ya wabunge na kupigwa shoka la kutimuliwa kutoka uongozi wa shughuli za serikali bungeni.

Ruto  alidinda mara mbili mualiko wa kuzungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa KICC lakini baadaye akatumia twitter kumtumia Duale ujumbe wa kumsifu na kumtaja kama kiongozi aliyejitolea kulihudumia taifa kwa  ukakamavu na kwa njia ya kipekee. Aliandika ;

“ Kaka yangu Aden Duale, wewe ni kiongozi shupavu. Kwa miaka minane umetekeleza majukumu yako vyema kama kiongozi wa wengi bungeni. Rafiki yangu, historia ya bunge ikiandikwa lazima  sura nzima itakuwa kukuhusu. Mbele iko sawa na Mungu’

Ruto hata hivyo hakumhongera mrithi wa  Duale Amos Kimunya ambaye aliteuliwa na rais Kenyatta kuichukua nafasi hiyo. Pia hakumtaja mbunge wa Eldas Adan Keynan ambaye ndiye katibu wa pamoja wa  Muungano wa Jubilee