Kinachomkwaza hata zaidi hadi leo ni kwamba mamake mzazi alikataa kumuamini kabisa kuhusu tukio ambalo hataki kulikumbuka. Ilikuwa baada ya kumaliza kidato cha nne miaka mitano iliyopita wakati Joy alipoamua kwenda kuishi na mamake kwa muda. Mamake alikuwa amemzaa kitambo na kurejea shuleni, kisha akaolewa baada ya kutoka shule huku Joy akilelewa na nyanyake wa kumzaa mama .
Alipomaliza shule, akiwa sasa anajiona kuwa mtu mzima alitaka kumjua mamake kwa undani na ndiposa akafiri lilikuwa jambo zuri kwenda kuishi naye kwa muda ili wafahamiene kama mtu na binti yake ingawa mamake alikuwa ashaolewa na mwanamme mwingine, ambaye sasa alikuwa babake wa kambo. Maisha yalikuwa mazuri na kila jambo likawa kama ilivyopangwa lakini siku moja likatokea tukio ambalo lilimbadilishia maisha na kumfanya kupoteza imani kabisa kwa kila mtu.
Siku moja Joy alipokuwa akienda bafuni kuoga, babake wa kambo alimfuata. Joy alishtuka na kupatwa na hofu kwa sababu mamake hakuwa nyumbani na jaribio lake kupiga kamsa halikumsaidia kwani jamaa alimfunika kinywa kwa taulo na kujilazimisha kwake. Alimbaka na kumuacha hoi kisha akenda zake. Joy alijizatiti na kusimama , akaoga na kisha akajifungia katika chumba chake. Mamake aliporejea, Joy alimueleza kilichofanyika lakini kwa mwelekeo ambao hakuna aliyeweza kutabiri, mamake hakumuamini na kumshtumu kwa kujaribu kumsingizia babake kambo kwa unyama huo. Mamake Joy hata aliendelea na kumshtumu binti yake kwa kujipepeza mbele ya mume wake kwa hatua alizodai zililenga kumnasa kitandani. Joy alihamakishwa kwamba alibakwa na babake kambo na mamake kwa kuzidisha makovu hakumuamini .
Tangia hapo, Joy alitoka na kurejea kwa nyanyake, akamsimulia kilichotokea. Nyanyake alimuamini na hadi leo yeye humueleza mamake Joy kwamba mume wake ni mnyamana na hafai kuwa naye. Lakini katu mama Joy ameendelea kumtetea mume wake akisema hawezi kumbaka binti yake. Kuna wanawake wengi ambao hata wameficha ushahidi dhidi ya wanaume wakatili ambao wametekeleza maovu kama ubakaji .Haijulikani iwapo ni mapenzi au kutekwa fikra lakini Joy anasumbuliwa na mawazo hadi leo kwamba mamake mzazi alichagua kumuamini mtu wa nje kumliko yeye .