Babu Owino- Katiba inafaa kubadilishwa na lazima Raila awe rais mwaka wa 2022

Mbunge wa Embakasi  Mashariki  Babu Owino amewataka wakenya kujitayaiosha kwa hatamu ya  Raila odinga kama rais baada ya kura ya  mwaka wa 2022. Mbunge huyo chipukizi  amesema wakati umewadia kwa katiba kurekebishwa ili kumaliza madhila ya uchaguzi na kuruhusu uongozi wa Raila Odinga .

Kupitia ujumbe wa Twitter ,Owino amesema wakenya wanafaa kujitokeza kwa  wingi ili kuunga mkono kura ya maoni na kumaliza migogoro ya kila wakati wa uchaguzi .Babu ni mfuasi mkubwa wa Raila  na amekuwa akikabiliana vikali na wote wanaompinga waziri mkuu huyo wa zamani . Ingawaje Odinga  hajatangaza nia ya kugombea urais mwaka wa  2022 , washirika wake wa karibu kama Babu wanaamini kwamba ndiye mgombeaji mkuu katika kipute hicho .

Matamshi kama hayo yamewahi kutolewa na Seneta wa Siaya James Orengo  na kakake Raila Oburu Odinga .

Baadhi ya viongozi walio katika mrengo wa naibu wa rais William Ruto  anayelenga kumrithi  rais Uhuru kenyatta  wamekuwa wakimshtumu Odinga kwa kuendeleza ajenda ya kurekebishwa katiba ili kujitengezea wadhifa wa uongozi serikalini.