Balala afutilia mbali uteuzi wa Pauline Njoroge kama mwanachama wa bodi ya mamlaka ya utalii

Waziri wa Utalii Najib Balala amefutilia mbali uteuzi wa Pauline Njoroge kama mwancahama wa bodi ya mamlaka ya kudhibiti shughuli za utalii nchini (Tourism Regulatory Authority).

Balala alitaja matamshi ya Njoroge ya awali kwa mitandao ya kijamii kuhusu mbuga ya wanyama ya Nairobi kuwa sababu ya kufutiliwa mbali kwa teuzi wake.

“Nafutilia mbali uteuzi wa Pauline Njoroge kama mwanachama wa bodi hii kwa sababu tumeona kwamba alikuwa ameandika kwenye twitter hapo nyuma kuwa mbuga ya wanyamana ya Nairobi haina manufaa,” Balala ananakiliwa kwenye taarifa ya wizara.

“Hatutaki kuhusishwa na watu kama hao na fikra hizo,” waziri alisema huku akieleza umuhimu wa wa mbuga ya wanyama ya Nairobi na kujitolewa kwa serikali kuilinda pamoja na maeneo mengine ya hifadhi za kitaifa.

Waziri kisha alitangaza kumteua mwanahabari Najma Ismail kuwa mwanachama wa bodi hiyo kuchukuwa nafasi ya Pauline Njoroge.

Mwanahabari Najma Ismail

“Tunasikitika kwamba hatukujua alichokuwa amesema hapo nyuma. Tunataka kuchukuwa nafasi hii kushukuru wakenya kakupitia mitandao ya kijamii kwa kufichua baadhi ya maelezo ambayo hatukuwa tumejua wakati wa kutafuta maelezo kumhusu,” taarifa hiyo ilisoma.

Njoroge alikuwa ameteuliwa pamoja na mwanawe kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kevin Musyoka, Alais Lenana na Isaac Njangu.