Baraza la Mawaziri lapiga marufuku raia wa kigeni kuasili watoto

baraza.la.mawaziri
baraza.la.mawaziri

Baraza la Mawaziri leo limepiga marufuku mara moja raia wa kigeni kuasili watoto hapa nchini.

Katika kikao maalum cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kuhudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto, baraza hilo  pia liliagiza Wizara ya Leba na Huduma za Jamii kubuni sera mpya za kuongoza uasili wa watoto na raia wa kigeni wanaoishi hapa nchini.

Kikao hicho pia kiliagiza wizara hiyo kulainisha shughuli za Shirika la kutetea Maslahi ya Watoto nchini na vile vile makao ya watoto hapa nchini.

Kuhusu muundomsingi, Baraza la Mawaziri liliidhinisha Shilingi bilioni 6.9 kwa ustawi wa Eneo la Kuhifadhia Makasha, Eneo la Shuguli za Kudhibiti mabehewa ya treni, Eneo la Usimamizi wa Mikakati ya Uchukuzi

na eneo la Matumizi ya  Umma.

Baraza hilo pia liliidhinisha muundomsingi muhimu wa kusaidia ujenzi wa Eneo Maalum la Kiuchumi la Naivasha pamoja na kukamilisha Awamu ya 2A ya Reli ya Kisasa (SGR).

Vilevile, Baraza la Mawaziri limeidhisha kuandaliwa kwa Kongamano la 25 Jijini Nairobi kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo.

Kongamano hilo ambalo litafanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 mwezi Novemba 2019 linatarajiwa kuvutia zaidi ya wajumbe 6,000 kutoka mataifa 179.

Kongamano hilo linatararajiwa kuitangaza Kenya na kuimarisha nafasi yake kuwa kituo muhimu cha kuandaa kongamano na uchukuzi wa ndege ili kuinua sekta ya utalii.

-PSCU