Bold or Dangerous? Rais Magufuli atangaza vyuo vikuu kufunguliwa Juni 1

Rais wa Tanzania John Pombe Magufui ametangaza kuwa vyuo vikuu vyote nchini humo vitafunguliwa kuanzia Juni 1, 2020.

Wanafunzi wa kidato cha sita nchini Tanzania ambao wanakaribia kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari nchini humo pia watarejea shuleni siku hiyo.

Magaufuli amesema kuwa wameamua kufanya hivyo kwa kuwa kasi ya ugonjwa wa corona imepungua nchini Tanzania.

"Hali ya ugonjwa wa Corona nchini imeshuka sana hivyo, sisi kama serikali tumeamua kufungua vyuo vyote Juni 1, 2020. Kwa hiyo, wizara zinazohusika zijiandae ili vyuo vitakapofunguliwa isitokee kero zingine," ameeleza Magufuli.

Magufuli hata hivyo amesema wanafunzi wengine bado kunahitajika muda wa kufanya tathmini.

"Kwa shule za msingi na madarasa mengine ya sekondari tujipe muda kidogo...tutatathmini maendeleo ya wengine waliofungua kwanza. Hawa wa chuo kikuu ni watu wazima, wanajitambua," amesisitiza rais Magufuli.

Taasisi zote za elimu nchini Tanzania zilifungwa katikati ya mwezi Machi mara baada ya Tanzania kuthibitisha mgonjwa wa kwanza wa virusi vya corona nchini humo.