Boni Khalwale atoa sababu za kujihami na mawe Kibra

Khalwale with stones
Khalwale with stones
Seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale amejitetea kwa nini alilazimika kujihami kwa mawe katika uchaguzi mdogo wa Kibra uliofanywa juma lililopita.

Khalwale alipigwa picha akiwa amejihami na mawe huku akikabiliana na umati uliokuwa unazua rabsha.

Seneta huyo wa zamani ambaye alikuwa amezuru Kibra ili 'kulinda kura' za mgombeaji wa Jubilee McDonald Mariga, aliwarushia mawe wahuni hao waliokuwa wamemkabili.

"Nilikuwa nimetulia  kisha takriban vijana 30 wakajitokeza wakiwa wamejihami kwa mawe. Nilikuwa jasiri na nilitaka kukabiliana nao kama mpiganaji wa mafahali kutoka Ikolomani," Khalwale alisema.

Akizungumza  mjini Kakamega Jumapili, Khalwale  alimlaumu waziri wa usalama wa ndani Fred Mating'i na Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai kwa utepetevu.

"Nawarai waziri Matiang'i na afisa mkuu wa polisi pamoja na katibu mkuu Karanja Kibicho kumakinikia suala la usalama wa wakenya," alisema.

Alilalamikia kuwa hata baada ya vurugu hizo, polisi  hawakuchukua hatua za kinidhamu kwa wahuni hao.

"Kwanini wakati wahuni  hao walikuwa wakizua rabsha hakuna yeyote aliyechukua hatua dhidi yao ? Polisi waliniacha nikipigania maisha yangu huku wakinitazama."

Khalwale alisema kwamba hakuwa na  nafasi nyingine ya kujisitiri  ila  kutumia mawe kuinusuru maisha yake.

"Mimi nikasikia hayo kupitia kwa mtandao kwamba ndio hao wanakuja..wakati walinikaribia, nataka musikie, hakunayeyote atakayewashurutisha Waluyha kuwapigia kura," alisema.

Khalwale alikuwa miongoni mwa  wanasiasa waliokuwa wakipigia debe mgombeaji wa Jubilee McDonald Mariga ambaye alishindwa na Imran Okoth wa ODM.