Kim Kardashian na Kanye West wakubaliana kutunza watoto pamoja baada ya kutalakiana

Muhtasari
  • Kanye West amekubali kutunza watoto wake wanne kwa ushirikiano na Kim Kardashian
  • Wamekubaliana kwamba hakuna kati yao anayehitaji msaada wa mwenzake

Kanye West amekubali kutunza watoto wake wanne kwa ushirikiano na Kim Kardashian.

Hatua yake inafuatia ombi la talaka lililowasilishwa na Kardashian tarehe 19 Februari, ambalo lilianzisha mchakato wa kumaliza ndoa yao ya karibu miaka saba.

Katika maombi yao wasanii hao wawili nyota, wamekubaliana kumaliza ndoa yao kufuatia tofauti ambazo haziwezi kusuluhishwa.

Wamekubaliana kwamba hakuna kati yao anayehitaji msaada wa mwenzake.

West na Kardashian wana mabinti wawili - North na Chicago, walio na umri wa miaka saba na mitatu - na wavulana wawili - Saint, miaka mitano, na Psalm, anaelekea kuwa na miezi miwili mwezi ujao.

Kwa mujibu wa ombi la Kardashian, walitenganisha mali zao wakati wote wa ndoa yao kutokana na makubaliano yaliofikiwa kabla ya kuoana.

Wanandoa hao ni miongoni mwa mastaa maarufu zaidi duniani wote wakipata ufanisi mkubwa kivyao. Ndoa yao imekuwa mojawapo ya zinazofuatiliwa kwa karibu katika miongo ya hivi karibuni.

Kardashian, 40, alipata umaarufu mwaka 2007 kama nyota kipindi cha uhalisia cha televisheni kuhusu familia yake, Keeping Up With The Kardashians.

Kipindi hicho kimekuwa maarufu tangu wakati huo ijapokuwa kinaelekea kukamilika katika kituo cha E! mwaka ujao.

Wiki iliyopita biashara zake kadhaa - ikiwemo ya urembo, mavazi na programu tumishi za simu -zilimfanya kupata hadhi ya bilionea duniani.

West, 43, ni mmoj wa watu wenye majina tajika katika ulimwengu wa muziki wa rap, na anatambuliwa kutokana na vibao kama vile Stronger, Jesus Walks na Gold Digger. Pia amepata ufanisi kama mwanamitindo wa nguo.

Mwaka uliopita, West aliwania urais wa Marekani japo hakufanikiwa. Wakati wa kampeni, mienendo ya rappa huyo hadharani na mitandaoni ilizua gumzo na kumfanya Kardashian kuzungumzia hali yake.

Alisema mume wake ana matatizo ya kiakili, na kuongeza kuwa "Ni mtu mwerevu lakini ni vigumu kumwelewa" na kutoa wito kwa watu kuacha kuangazia hali yake mitandaoni na katika vyombo vya habari.